2015-04-08 09:56:00

Pasaka iliyosheheni majonzi makubwa nchini Kenya: Changamoto ni umoja!


Viongozi wa kidini nchini Kenya wametumia kipindi cha siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wanafunzi 150 waliouwawa kikatili kutokana na shambulizi la kigaidi lililofanywa na Al Shabaab. Katika maadhimisho ya Pasaka, Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya alisoma salam za rambi rambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu ameitaka Familia ya Mungu nchini Kenya, licha ya changamoto zote hizi kuendelea kujikita katika mchakato utakaodumisha haki, amani na usalama.

Kardinali Njue kwa upande wake amewataka wananchi wa Kenya na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia, kuunganisha nguvu katika mapambano dhidi  ya ugaidi, jambo ambalo kwa sasa limekuwa ni tishio kubwa la usalama na maisha ya watu wengi. Wananchi wa Kenya hawana budi kuendelea kushikamana katika umoja, udugu na upendo na kamwe wasiruhusu kugubikwa na chuki pamoja na uhasama wa kidini na kudhani kwamba, haya ni mapambano kati ya Waislam na Wakristo nchini Kenya.

Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amewataka wakenya kushikana mkono na kusaidiana , changamoto kwa Serikali kuhakisha usalama wa maisha ya raia na mali zao, ingawa shambulio hili lingeweza kudhibitiwa ikiwa kama Serikali ingekuwa makini bila kupuuza onyo lililokuwa limetolewa na baadhi ya nchi kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi nchini Kenya.

Askofu mkuu Eliud Wabukala wa Kanisa Anglikani, Kenya amesema kwamba, magaidi wanataka kuwagawa wananchi wa Kenya kwa misingi ya udini, lakini watambue kwamba, hawataweza kufanikisha azma hii, kumbe Wakenya waendelee kushikamana kwa dhati. Amewasahuri viongozi wa Kiislam nchini Kenya, kuhakikisha kwamba, wanatoa malezi makini kwa waamini wao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wanaosimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, utu na heshima ya binadamu sanjari na mfungamano wa kijamii.

Viongozi mbali mbali wa Jumuiya za Kiislam nchini Kenya wao pia wamelaani sana vitendo vya kigaidi vilivyofanywa mjini Garissa na kupelekea wanafunzi 150 kupoteza maisha yao na wengine wengi kupata majeraha makubwa. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.