2015-04-08 10:44:00

Kuna watoto ambao wamebaki Ijumaa kuu: wanateseka na kunyanyasika sana


Baada ya pilika pilika za maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 8 Aprili 2015 ameendelea na katekesi yake kuhusu familia kwa kuchambua kwa kina na mapana watoto ambao ni zawadi na baraka kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini wengi wa watoto hawa bado wako Ijumaa kuu, wakiendelea kuteseka, kunyanyasika na kupokwa matumaini ya maisha bora.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kuna watoto tangu siku yao ya kwanza kutungwa mimba, wanakataliwa, wanatelekezwa na kupokwa hali yao ya maisha ya utoto kiasi cha kuharibu matumaini ya maisha yao kwa siku za usoni. Kuna baadhi ya watu wanasema kuzaa watoto duniani ni kosa kubwa kutokana na udhaifu wao, njaa na magonjwa yanayowaandama.

Baba Mtakatifu anasema, si kosa hata kidogo watoto kuzaliwa duniani kwani shida, mateso na mahangaiko yao yanapaswa kuwa ni sababu ya kuwapenda zaidi. Kila mtoto anayeishi na kuomba omba barabarani ananyimwa haki ya kusoma na kupata tiba makini, hiki ni kilio cha uchungu mbele ya Mwenyezi Mungu. Mara nyingi watoto hawa wanakuwa ni wahanga wa vitendo vya uhalifu na kuna baadhi ya watu wanaowatumia kwa biashara au katika vitendo vya kihalifu.

Baba Mtakatifu anaendelea kubainisha kwamba, hata watoto wanaoishi kwenye Nchi zilizoendelea duniani wanakabiliwa na magumu katika maisha kutokana na kinzani na myumbo wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Mambo yote haya yanaathiri utoto wao kiroho na kimwili. Yesu aliwaalika wanafunzi wake kuwaachia nafasi watoto ili waje kwake, kwani Ufalme wa mbinguni ni kwa ajili ya watu kama hawa, yaani wanyenyekevu.

Hivi ndivyo Yesu anavyowaaminisha wazazi. Kuna wazazi wengi ambao kila siku wanaendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao. Kanisa kwa upande wake, linatoa upendo wa kimama kwa watoto na familia zao na kuwapatia baraka kutoka kwa Yesu Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha daima upendo kwa watoto bila kuhesababu gharama na kamwe wasijisikie na kuamini kwamba, wao ni mzigo kwa jamii, bali kito cha thamani mbele ya Mungu na mwanadamu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwa mashuhuda amini wa upendo na huruma ya Mungu kwa wote katika medani mbali mbali za maisha yao. Ni mwaliko wa kuwahudumia watoto kama sehemu ya mchakato wa kuwekeza katika maisha yao kwa kuwapokea na kuwapenda.

Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anawasalimia mahujaji kutoka Iraq na Mashariki ya Kati katika ujumla wao, amekumbusha kwamba, mara nyingi watoto ndio waathirika wakuu wa kinzani za kifamilia, vita na madhulumu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwaombea watoto ili waweze kupata ulinzi na tunza kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ageuze mioyo ya jiwe ili iweze kuonesha upendo kwa watoto. Anaendelea kuwatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema neema, baraka na amani kutoka kwa Kristo Mfufuka. Anawashukuru waamini wote kwa sala, salam na matashi mema waliyomtumia wakati wa Pasaka.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu; anapenda kuwafariji wote wanaoteseka kutokana na shida mbali mbali. Waamini kwa ari, upendo na moyo mkuu, wawe tayari kushiriki katika ujenzi wa dunia ambamo wanaishi; kwa kushirki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wajitahidi kulea ujana wao kwa kujikita katika majiundo makini, ili kuendelea kuwa na nafasi ya pekee mbele ya Yesu Kristo aliyewakomboa kutoka katika dhambi na mauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.