2015-04-08 09:47:00

Hija ya kitume miongoni mwa wakimbizi nchini Iraq!


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu amehitimisha hija ya kichungaji nchini Iraq, ambako amepata fursa ya kuadhimisha Mafumbo makuu ya Kanisa akiwa kati ya wakimbizi na wahamiaji, kama kielelezo makini cha upendo na mshikamano wa kidugu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati wanaonyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi.

Kardinali Filoni anabainisha kwamba, ziara hii imekuwa ni hija ambayo imeacha utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho; amewaonjesha Wakristo imani na matumaini, licha ya shida na mahangaiko wanayokabiliana nayo kwa sasa. Amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Kanisa mahalia na kuadhimisha kwa pamoja Mafumbo ya maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Filoni ametembelea na kuangalia mazingira ya kambi za wakimbizi na wahamiaji; hali si nzuri sana, lakini walau watu wanapata hifadhi ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasaidia kulinda na kutetea maisha na haki msingi za Wakristo wanaoendelea kuuwawa kikatili huko Mashariki ya Kati. Huu ni umati mkubwa wa mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake kwa nyakati hizi anasema Baba Mtakatifu Francisko. Mauaji na nyanyaso dhidi ya Wakristo kwa misingi ya imani kali za kidini ni jambo lisilokubalika kamwe, ingawa linaendelea kufumbiwa macho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.