2015-04-08 14:38:00

Epuka maradhi kwa kujali kila kinachoingia kinywani mwako!


(Vatican Radio) Jumanne  7 April ilikuwa Siku ya Afya  Duniani." Unatakiwa kujali kila unachokula kwa kuwa kinaingia mwilini mwako !“ Ni angalisho lililotolewa katika kuadhimisha siku ya Afya ya Dunia kwa mwaka huu, adhimisho la kila tarehe 7 Aprili kama ilivyoteuliwa na Umoja wa Mataifa .  Mwaka huu adhimisho lililenga zaidi katika  usalama wa chakula , tangu kinapozalishwa  hadi kinapomfikia mlaji mezani. Shirika la Afya la Dunia "WHO",limetoa hoja hiyo kama kujali  ongezeko kubwa na maradhi yanayotokana na chakula kibovu.

Shirika la Afya Duniani, linaitaja  Siku hii  7 Aprili, kuwa  fursa ya kuuelimisha umma,  changamoto na matatizo yanayohusiana na  ukosefu wa chakula salama. Kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa "Kutoka shambani hadi katika  sahani, fanya  chakula salama”. Takwimu mpya za madhara yanayosababishwa na magonjwa yanayo tokana na chakula zimekuwa ni  kitisho cha kimataifa, na hivyo kuzua haja ya  kuwa na uratibu wa karibu katika mlolongo mzima wa hatua zote zinazo hitajika  tangu uzalishaji na  usambazaji chakula hadi kinywani kwa mlaji.

Dr Kazuaki Miyagishima, Mkurugenzi wa Shirika kwa ajili ya Usalama wa chakula katika  Idara ya Elimu ya Afya katika  Umoja wa Mataifa,  anasema  usalama wa chakula ni tatizo kubwa katika  afya ya umma. Leo hii chakula si salama kutokana na kuchafuliwa na mambo mengi kama  virusi, bakteria, vimelea na kemikali, na kusababisha zaidi ya magonjwa  200 mbalimbali. Na hivyo  Sekta mbalimbali zinazo husiana na shughuli zinazo gusa chakula, kama vile kilimo, uvuvi, viwanda, utalii, biashara, vinapaswa kushirikiana kwa ajili ya kuhakikisha chakula kinakuwa ni salama katika hatua zake zote hadi kinapofika katika kinywa cha mlaji.

 Pia ujumbe wa Mkurugenzi Mkuu Dr Margaret Chan wa WHO, unasema, katika mazingira ya utandawazi , hasa biashara huria iliyotengeneza  fursa nyingi mpya  hasa katika usambazaji wa haraka wa chakula, imetoa pia mianya mingi ya  kusambaa kwa haraka  vimelea na bakteria wa  hatari na chakula kilichofuliwa na kemikali.  Na hivyo  sasa tatizo la usalama wa chakula la mitaani kwa haraka linasambaa kwa haraka sana na kuwa dharura ya kimataifa.  Na kuzuka kwa ugonjwa unaotokana na chakula, linakuwa ni tatizo ngumu  kutatua kwa kuwa chakula kilichoko katika  sahani moja au kutoka katika paketi moja ya chakula kutoka nchi nyingine, inakuwa ni kazi kubwa kufuatilia asili ya chakula kilipotoka.

Chakula kisicho salama hudhuru kwa uwepo wa  bakteria, virusi, vimelea au kemikali , ikisababisha aima mbalimbali za maradhi tangu kuharisha, hadi saratani. Mifano ya vyakula visivyo salama ni kama vile vinavyoliwa bila  kupikwa,  vyakula vyenye  asili ya wanyama, matunda na mboga zilizolimwa katika mazingira machafu au kutoteshwa kwa kutumia mbolea ya  kinyesi, na  pia samakigamba waliouawa kwa sumu na kuvuliwa baharini, na watu wenye uchu wa fedha za harakaharaka .

Taarifa inaendelea kutoa mfano  vijidudu  aina ya Salmonella Typhi , husababisha  wastani wa vifo 52,000, wakati  aina ya E. coli huua wastani wa watu  37, 000, na norovirus  huua  watu 35,000 kwa mwaka. Na kwamba, idadi kubwa ya maradhi yanayotokana na chakula na vifo hutokea  Afrika ikifuatiwa na  Kusini-Mashariki mwa Asia na zaidi ya 40% ya watu wanaosumbuliwa na maradhi haya yanayosababishwa na chakula kichafu ni  watoto wenye umri chini ya miaka 5.

Hivyo WHO, linafanya jitihada za kidharura, kwa ajili ya kufanikisha  njia za maendeleo chanya katika  mifumo mikubwa ya usalama wa chakula, kwa kuhusisha  serikali  na hatua za umma katika  kulinda  chakula  dhidi ya uchafuzi kemikali au vijidudu au virusi. WHO inachukua hatua madhubuti  kitaifa na kimataifa, katika ufanikishaji wa  jukumu muhimu hili muhimu katika kukuza usalama wa chakula tangu shambani hadi mezani,Ofisi ya habari ya  WHO imeripoti. 

imehaririwa na tjmhella -Radio Vatican 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.