2015-04-07 10:55:00

Wakristo shikamaneni katika kweli za Kimungu, maadili na utu wema!


Patriaki Kirill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima katika maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa mwaka huu 2015 ametuma ujumbe wa matashi mema kwa viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko. Anasema kwamba, Kanisa linaadhimisha Siku kuu  ya wokovu kwani Yesu Kristo amefufuka katika wafu!

Ufufuko wa Kristo unaonesha mwanga angavu ambao kwa njia ya mauti amemharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi. Kanisa linamwimbia Kristo utenzi wa sifa na shukrani, kwa wema na ukarimu wake kwa binadamu, changamoto ya kuimarisha umoja na ushirikiano kati ya Wakristo mintarafu ushindi wa ukweli kuhusu Mwenyezi Mungu. Ni mwaliko wa kuimarisha matendo ya upendo yanayobubujika kutoka katika misingi ya Kiinjili; wema na huruma; tunu msingi za maisha ya kiroho na kimaadili.

Patriaki Kiril anasema, Mwenyezi Mungu muumbaji na mwingi wa hekima ambaye kwa rehema zake nyingi amewazaa mara ya pili, ili wapate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu, ili wapate urithi usioharibika, usio na uchafu wala kuweza kunyauka. Mwenyezi Mungu awalinde katika nguvu ya mwili na roho na kuwakirimia wema na ukarimu wake usiokuwa na mipaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.