2015-04-07 10:07:00

Mchango wa mashirika ya kitawa katika maisha na utume wa Kanisa Afrika


Watawa ni walinzi na watetezi wa zawadi ya uhai;  ni wadau na watekelezaji wakuu wa mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Watawa  ni kundi linaloponya, linalolea, tetea na kuimarisha imani. Ni watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasikiliza na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa wako kati ya Watu wa Mungu ili kuwatia shime na kuwaimrisha katika imani, matumaini na mapendo.

Kwa muhtasari hii ndiyo dhamana inayotekelezwa na Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee Barani Afrika kama anavyobainisha Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu katika mahojiano maalum na Radio Vatican, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani.  Mashirika mengi Barani Afrika yanaendelea kuadhimisha Jubilee ya miaka 50, 75 na mengine 100 tangu yalipoanzishwa.

Sr. Maria Ugenia Thomas anabainisha kwamba, watawa wamekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma makini kwenye sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii na matunda ya majitoleo haya yanaonekana sehemu mbali mbali za dunia. Watawa wamekuwa wasaidizi wakuu wa Mapadre na Maaskofu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.