2015-04-07 09:11:00

Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa: Rejeeni kwa Kristo: Jana, Leo na Daima


Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani yaliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko ni mwaliko kwa watawa kupyaisha tena maisha na utume wao, kwa kufanya rejea makini kwa nyaraka zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu maisha na utume wa Watawa ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, watawa wasome na kutafakari Waraka kuhusu Mapendo kamili, Perfectae caritatis.

Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kujikita katika mchakato unaolenga kuyapyaisha maisha na utume wao kadiri ya maisha na changamoto zinazotolewa na Yesu Kristo aliyekuwa mtii, fukara na mseja; Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Yesu aliweza kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu mintarafu mpango wa Mungu; akautakatifuza muda na kuufanya kuwa ni Sakramenti ya Upyaisho wa maisha na makuzi ya kiroho.

Hili ndilo lengo kuu katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, unaoendelea kupamba moto sehemu mbali mbali za dunia. Haya yamesema hivi karibuni na Padre Sostenes Luyembe, SJ. Mwakilishi wa Askofu mkuu kwa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, Jimbo kuu la Dodoma katika Ibada ya Misa takatifu kama sehemu ya ufunguzi wa maadhimisho ya Mwaka wa Watawa, Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania.

Watawa wanapaswa kumrejea Yesu Kristo, jana, leo na daima kwa kutambua kwamba, Jimbo kuu la Dodoma limebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa watawa kutoka katika Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume, wanaounganika na kujumuika kwa pamoja, ili kuleta harufu nzuri na yenye mvuto katika maisha na utume wa Kanisa, Jimbo kuu la Dodoma. Jambo la msingi anasema Padre Luyembe ni kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na udugu.

Padre Luyembe anasema kwama, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza watawa katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani; kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Watawa wafanye tafakari ya kina kwa kurejea katika maisha, malengo na karama za waasisi wa Mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume ili kujibu changamoto za Uinjilishaji katika ulimwengu mamboleo na kwa namna ya pekee katika Jimbo kuu la Dodoma, ili kuweza kuitangazia Familia ya Mungu, Injili ya furaha, matumaini na mapendo kwa njia ya huduma makini! Watawa waundwe na kufundwa barabara na historia na karama za mashirika yao, ili kupata utambulisho unaoimarishwa katika umoja na mshikamano kwa kutambua kwamba, wao pia ni sehemu ya Familia ya Mungu, wanahitaji kusoma alama za nyakati, ili kujibu mahitaji ya watu wa nyakati hizi.

Padre Luyembe anawataka watawa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza na hatimaye, kumwilisha karama za mashirika yao kwa kupambana nachangamoto mbali mbali ambazo zinaweza kukwamisha mchakato huu ili usiweze kupata mafanikio yake. Watawa wawe ni waaminifu kwa karama za mashirika yao pamoja na mashauri ya Kiinjili. Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa iwe ni fursa ya kuishi kikamilifu Injili ya Kristo. Hii ndiyo Leo anayozungumzia Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Padre Sostenes Luyembe, anawasihi watawa kutafakari kesho kwa kuangalia changamoto zinazotishia maisha na utume wa mashirika haya ya kitawa na kazi za kitume, kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa. Miito inazidi kupungua, watawa wanazidi kubwaga manyanga kila mwaka; wazee na wagonjwa wanazidi kuongezeka maradufu; misaada kutoka ng’ambo inazidi kukauka na kunyauka; hali ya uchumi ni mbaya, ukata unaendelea kutishia maisha; utandawazi na athari zake vinatishia tunu msingi za maisha ya kitawa; kuna kinzani na migogoro ya kidini na kijamii; mambo yote haya yanawagusa watawa katika maisha na utume wao!

Lakini wanapaswa kuwa na moyo mkuu na kamwe wasikate tamaa kwani yesu mwenyewe anasema yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali. Watawa wajenge ujasiri wa kusonga mbele huku wakipigana bila kushindwa. Watawa wasigeuze nyumba za kitawa kuwa ni kichaka cha wivu, majungu, umbea na unafiki. Kila mtawa atambue kwamba ndani mwake kuna mapambano kati ya mwanga na giza; mambo yanayohitaji ukuaji na ukomavu; kuna kufanikiwa na kushindwa katika maisha; lakini watawa wasikate tamaa, bali watambue yote haya na kuendelea kuwa ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini, daima wakimwangalia Yesu Kristo pale juu Msalabani!

Na Padre Sostenes Luyembe, SJ.

Jimbo kuu la Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.