2015-04-05 11:07:00

Kesha la Pasaka: Kumbu kumbu kwa wakristo wanaoteseka, wasikate tamaa!


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi kuu, tarehe 4 Aprili 2015, ameadhimisha Ibada ya Kesha la Pasaka, mama ya makesha yote yanayoadhimishwa na Kanisa, kwa: Ibada ya kubariki moto na kuingia kwenye Kanisa kuu kwa maandamano yaliyoongozwa na Mshumaa wa Pasaka, kielelezo cha Kristo Mfufuka pamoja na kuimba Mbiu ya Pasaka, mashangilio makuu kwa ajili ya Kristo Mfufuka. Ibada hii ya Misa Takatifu imeanza kunako majira ya saa 2: 30 Usiku kwa saa za Ulaya.

Baba Mtakatifu ametoa Sakramenti ya Ubatizo kwa Wakatekumeni 10 na kuwaimarisha pia kwa Sakramenti ya Kipaimara, tayari kumshuhudia Kristo katika maisha yao ya kila siku. Hawa ni waamini kutoka Italia, Albania na Ureno. Licha ya Liturujia ya Kesha la Pasaka kutangaza furaha ya ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti, lakini kwa mwaka huu, imekuwa ni fursa pia ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaoendelea kuteseka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kanisa limesali kwa ajili ya kuwaombea pia viongozi na wadau mbali mbali wanaoendelea kujibidisha ili kutafuta haki, amani na upatanisho sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa amewaombea toba na wongofu wa ndani wale wote wanaopandikiza mbegu ya kifo na hofu, ili waweze kutubu na jatimaye kumwongokea Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya haki na amani. Waamini wanahamasishwa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.

Siku kuu ya Pasaka, asubuhi, tarehe 5 Aprili 2015, Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ambayo imehudhuriwa na umati mkubwa wa waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hali ya hewa ilikuwa mbaya, lakini watu wamevumilia hadi mwisho na kusikiliza pia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya mji wa Roma na Dunia kwa ujumla kama unavyojulikana kwa lugha ya Kilatini “Urbi et Orbi”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.