2015-04-04 08:30:00

Pasaka ni kielelezo cha utukufu, amani na upendo wa Mungu kwa binadamu


Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu! Ni salam na matashi mema kutoka kwa viongozi wakuu wa Makanisa Nchi Takatifu, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe za Pasaka, yaani ufufuko wa Yesu Kristo.

Ni salam zenye imani na matumaini licha ya vita, mateso na nyanyaso zinazoendelea kuhatarisha na kudhalilisha maisha ya mwanadamu, lakini Wakristo wana matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa, utambulisho unaoipamba Nchi Takatifu, chimbuko la Ukristo. Hapa ni mahali ambapo kunapatikana Kaburi tupu, linaoonesha utukufu wa Mungu dhidi ya Fumbo la kifo na mauti, eneo la ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu na wala si mahali pa kuzima kiu ya udadisi wa binadamu. Na ugunduzi wa mambo ya kale!

Yerusalem ni kielelezo cha imani hai ya Wakristo. Hapa ni mahali ambapo neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu zimejionesha kwa miaka mingi, eneo linalohitaji kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Viongozi wa Makanisa Nchi takatifu wanapenda kuungana na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha masikitiko yao kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma inayoendelea kufanyika huko Mashariki ya KatiĀ  na sehemu mbali mbali za dunia kwa kisingizio cha udini.

Wakristo huko Iraq, Syria na Misri ni watu ambao wanaathirika vibaya zaidi kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati. Hakuna dini ya kweli inayoweza kujikita katika vita, nyanyaso na dhuluma dhidi ya binadamu au kundi la watu wachache kwa misingi ya kiimani. Wakuu wa Makanisa wanapenda kuchukua nafasi kulaani vitendo vyote vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wanawaomba Wakristo huko Mashariki ya Kati kuto kata tamaa kwani uwepo wa Mji wa Yerusalem ni kielelezo cha mwanga na matumaini mapya yanayojikita katika misingi ya haki, amani, upendo na kwamba, iko siku haki ya Mungu itashinda.

Viongozi wa Makanisa wanasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wamezungukwa na uvuli wa mauti, shaka na giza; mambo yanayowafanya wakristo wengi kutoweza kuadhimisha Fumbo la Pasaka kwa furaha na shangwela. Lakini hakuna sababu ya kukata tamaa, huu ni mwanzo wa mapambazuko mapya, yaani ile Siku ya kwanza ya Juma, Yesu alipofufuka kutoka katika wafu, akashinda dhambi na mauti.

Vita, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo ni mambo ambayo si hatima katika maisha yao, bali ni upendo, haki na matumaini kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yesu Kristo aliyefufuka kutoka katika wafu siku moja atakuwa yote katika yote wakati wa utimilifu wa Ufalme wa Mungu. Viongozi wa Makanisa katika Nchi Takatifu wanahitimisha ujumbe wao wa Pasaka kwa kusema kwamba, kwa hakika Bwana Yesu amefufuka kweli kweli, Alleluiya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.