2015-04-04 09:22:00

PASAKA: Iko siku, amani itachipuka na kutawala mioyoni mwa watu!


Pasaka ni Fumbo ambalo limegharimu maisha na uhuru, kiasi hata cha Yesu Kristo kujisadaka kwa njia ya mateso na kifo cha aibu, ili aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Fumbo la Pasaka linaonesha kile kipindi cha mpito na upya wa maisha unaojikita katika toba na wongofu wa ndani. Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya maisha mapya, ushindi wa Injili ya Uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo, haya ni mapambano endelevu katika maisha ya mwamini.

Askofu mkuu Santo Marcianò wa Jimbo la Kijeshi Italia anasema vita ni adui mkubwa ambaye anapaswa kuvaliwa njuga na watu wote wenye mapenzi mema, kwani vita kwa kawaida inabeba ndani mwake, nyanyaso, dhuluma na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, matukio yanayoendelea kufanywa na vikundi vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Haya mapambano hayana budi kuelekezwa dhidi ya utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, ubaguzi wa rangi na kidini; nyanyaso na dhuluma dhidi ya utu na heshima ya binadamu, lengo ni kuhakikisha kwamba, amani ya kweli inatawala katika maisha na mioyo ya watu.

Askofu mkuu Marcianò anasema, hata pale amani inapoonekana kana kwamba, imetoweka, lakini inaweza kuibuka taratibu kwani huu ni mchakato unaopaswa kujikita katika undani wa mwanadamu, katika hali ya ukimya; huduma, majadiliano na kushirikishana fadhila mbali mbali katika maisha. Amani inaweza kupatikana kwa njia ya sadaka na majitoleo ya watu wanaopania kweli kujenga amani kwa ajili ya mafao ya wengi.

Katika mazingira ya watu wengi amani na matumaini vinaonekana kana kwamba, vimetoweka kutokana na kushamiri kwa vitendo vya kigaidi, vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Ni mauaji yanayoendelea kutendwa kwa misingi ya kiimani, kinyume kabisa cha utashi na mapenzi ya Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya maisha, ndiyo maana Mama Kanisa anatumwa kutangaza Injili ya Uhai hadi miisho ya dunia. Amani ni jibu makini kwa mashuhuda wa imani wanaoendelea kila siku kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kutokana na mashambulizi ya kigaidi na vita ya kidini.

Pamoja na matukio yote haya Askofu mkuu Marcianò anasema, iko siku amani itatawala katika mioyo ya watu. Amani itachipua kutoka katika kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia; kutoka kwa wale wanaoendelea kusimama kidete kuilinda na kutetea amani hata kiasi cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya mafao ya wengi; amani itachipua kutokana na sala za waamini wanaomlilia Mungu kila siku ya maisha yao na kwamba, uhakika wa amani ni Fumbo la Pasaka. Hii ndiyo zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kumkirimia mwanadamu katika maisha yake! Maisha mapya yanabubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba, baada ya Ijumaa kuu kuna shangwela la Pasaka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.