2015-04-04 13:55:00

Ekaristi Takatifu ni maisha ya kujisadaka!


Tangu zamani za kale Waisraeli walitolea sadaka za wanyama na mazao kama alama ya shukrani. Hata wakati waisraeli walipotoka utumwani Misri ibada ya pasaka na sikukuu ya mkate isiyochachwa ikaunganishwa na kuadhimishwa sasa kama sadaka moja ya ibada ya wokovu, ikifanyika sasa kukumbuka walipotoka utumwani Misri. Tangu zama hizo hata leo bado wanadhimisha ibada hii. Wakati wa Kristo, mwanakondoo wa Mungu amejidhabihu msalabani akajitoa kama chakula katika karamu ya mwisho katika juma la pasaka ya waisaraeli. Tunaadhimisha ibada hiyo kila mwaka katika juma kuu. Kristo ameiletea dunia yote wokovu kwa karamu yake na msalaba wake. Kadiri ya imani yetu, tendo lile lile la karamu na msalaba linaendelezwa na Kristo katika misa takatifu iliyo karamu na sadaka ile ile ya Kristo.

 

Karamu (chakula cha) ya bwana maana yake ni Ekaristi Takatifu. Karamu hii ni ukumbusho wa karamu ya mwisho ya Bawana pamoja na mitumume waleke alipoweka Ekaristi Takatifu. Mapokeo fulani ya Kiyahudi yalieleza neno pasaka kwa maana ya kuvuka, yaani kuvuka bahari ya Shamu - kut. 14. Kristo na sisi pamoja naye tutauvuka ulimwengu huu wa dhambi na kwenda kwa Baba katika nchi ya ahadi – Kut. 21. Kristo ameshatuvusha, hivyo ni juhudi na bidii yetu kubaki pamoja naye ili tufike tuendako. Ili tufike kwa Baba yahitajika juhudi binafsi, juhudi ya jamii inayoamini - walipo wawili au watatu kwa jina langu nami nipo kati yao. Lakini zaidi sana yahitajika neema ya Mungu ili tuweze kufika kwake.

 

JUU YA KARAMU YA PASAKA.

 

Kadiri ya wainjili Matayo, Marko, na Luka,  Yesu alifanya karamu ya pasaka siku ya alhamisi jioni – Mt. 26:17, Mk. 14:12, Lk.22:7. Yesu alipokula karamu ya Pasaka jioni ile aliweka ibada mpa ya karamu. Katika kuweka karamu mpya katikati ya karamu ya Pasaka, Yesu alidokeza kwamba ibada yake mpya ni utimilizo wa pasaka ya kale - karamu ya Bwana  au chakula cha bwana maana yake ni ekaristi takatifu -1Kor.11:20. Karamu hii ni ukumbusho wa karamu ya mwisho ya Bwana pamoja na mitume wake alipoweka ekaristi takatifu. Nayo inakumbusha kifo cha Yesu, tena ni amana ya karamu ya kimasiya - siku za mwisho  - Mt. 26:29, Md. 2:42 - wakawa wakidumu katika fundisho la mitume na katika ushirika na katika kuumega mkate na katika kusali. Katika tendo hili kuu na takatifu, Yesu aliweka sakramenti ya daraja, sakramenti ya ekaristi na pia amri ya Bwana ya kupendana.

SAKRAMENTI YA DARAJA

 

Katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki tunasoma hivi;

Na. 1539 - taifa teule liliwekwa na Mungu kama ufalme wa makuhani na taifa takatifu lakini ndani ya taifa la Israeli Mungu alichagua moja ya makabila kumi na mawili, lile la Walawi akalitenga kwa ajili ya huduma ya liturujia. Mungu mwenyewe ni fungu la urithi wake. Ibada ya pekee ilitakasa mianzo ya huduma ya liturjia. Mungu mwenyewe ni fungu la urithi wake. Ibada ya pekee ilitakasa mianzo ya ukuhani wa agano la kale. Ndani yake makuhani waliwekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu ili kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi – Ebr. 5:1, Kut. 29:1-30, Law. 8.

 

Na. 1540 - ukuhani huu uliwekwa kwa ajili ya kutangaza neno la Mungu - Mal. 2:27-29 na kwa ajili ya kurudisha uhusiano pamoja na Mungu kwa sadaka na sala. Hata hivyo unabaki hauna nguvu ya kuleta wokovu ukiwa na lazima ya kurudia sadaka zake bila kukoma na kutoweza kutoa utakaso halisi ambao ungetimizwa tu na sadaka ya Kristo – Ebr. 5:3, 7:27,10:1-4.

 

    Kwa kifupi sakramenti ya daraja ni sakramenti ya upendo. Ili sakramenti ya ekaristi iliendelee kuadhimishwa ni lazima wawepo mapadre ambao kwa dhamana waliyopewa wanaweza kugeuza mkate na divai kuwa mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.

 

SAKRAMENTI YA EKARISTI

 

Na. 1322 - Ekaristi Takatifu hukamilisha kuingizwa katika ukristo wale walioinuliwa katika heshima ya ukuhani wa kifalme kwa ubatizo na kufananishwa kwa ndani zaidi na Kristo na kwa kipaimara hushiriki pamoja na jumuiya yote katika sadaka moja ya Bwana.

 

Na. 1323 - mwokozi wetu katika karamu ya mwisho usiku alipotolewa aliweka sadaka ya ekaristi ya mwili na damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie bibi arusi mpendwa yaani kanisa ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya pasaka ambamo Kristo huliwa na roho hujazwa neema na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele.

Na. 1324 - Ekaristi ni chemichemi na kilele cha maisha yote ya kikristo. Sakramenti nyingine kama zilizo pia huduma zote za kanisa na kazi za utume zaungana na ekaristi na zaelekezwa kwake. Kwani katika ekaristi takatifu mna kila hazina ya kiroho ya kanisa yaani kristo mwenyewe pasaka wetu.

Na. 1325 - Ekaristi ndio ishara thabiti na sababu ya hali ya juu kabisa ya ushirika katika uzima wa kimungu na umoja ule wa taifa la Mungu ambao unalifanya kanisa liwepo ekaristi ni kilele cha tendo la Mungu la kuutakatifuza ulimwengu katika kristo na kilele cha tendo la kumwabudu Mungu wampalo watu kristo na kwa njia yake wampalo baba katika mtakatifu.

Na. - 1326 - mwishowe kwa njia ya adhmisho la ekaristi tunaungana tayari sisi wenyewe na liturjia ya mbinguni na tunaanza kutangualia kushiriki uzima wa milele Mungu atakapokuwa yote katika wote - 1 Kor. 15:28 - basi vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake ndipo mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiisha vitu vyote ili kwamba Mungu awe yote katika wote.

 

Na. - 1327 - kwa ufupi ekaristi ndiyo juma na muhtasari wa imani yetu, namna yetu ya kufikiri hulingana na ekaristi na ekaristi kwa zamu yake huimarisha namna yetu ya kufikiri.

 

 

 

MAHUBIRI YANAJIKITA KATIKA VIFUNGU VIFUATAVYO:

  1. KUT. 12:1-8,11-14
  2. 1 KOR. 11: 23-26
  3. YOH. 11:13,1-5

 

Mazingira ya nchi ya Israeli na makazi - umbali na ugumu wa njia – msafiri alipofika au bado akiwa safarini alihitaji kupumzika na katika kupumzika huko alihitaji kuoshwa miguu na kupewa chakula. Hiyo ndiyo ilikuwa desturi ya wenyeji. Mapumziko haya yalihitajika ili kupata nguvu ya kuendelea na safari baadaye au kesho yake baada ya mapumziko hayo.

 

Ekaristi Takatifu yachukua nafasi hiyo sasa. Maisha ya mkristo hapa duniani ni sawa na safari ndefu na ngumu. Safari ya kwenda mbinguni kwenye makao ya milele. Njiani tunachoka na kunyauka hata kupata kishawishi cha kutaka kukata tamaa. Leo hii bado kishawishi hiki kipo. Lakini twaona kuwa Yesu katufutilia mbali ugumu huo na leo hii anatupatia ekaristi, pumziko letu - ndani yake tunapata  muda wa kunawa miguu na kupata chakula cha mwili na roho tayari kuendelea na safari yetu iliyo mbele yetu tena ngumu, ya kwenda juu kwa baba. Ekaristi daima ni viaticum au nguvu ya safari kwani tunapata nguvu ya kuendelea na safari yetu kwenda juu.Mambo yanayofanyika ni kukaa pamoja mezani, kula na kunywa pamoja na kuagana na kwa mifano hai n.k. Tendo la kuosha miguu - Mtume Petro anasita na angependa yeye afanye jambo hilo kwa Yesu. Jibu la Yesu - mimi nitakuosha miguu wewe - Yoh .13:8.

Kwanza Yesu anatuosha sisi na uchafu wetu ili tuwe watu wake,

 

CHANGAMOTO

Ekaristi ni maisha, ni uhai, ni upendo - kujigawa vipande, kuwaosha wengine, kubariki kazi zao nzuri, kuanza upya, kuvuka vizingiti ya makwazo, ni wajibu na zaidi sana ni fumbo. Tusipoteze muda wetu kutaka kulielewa fumbo hili kwa akili ya kibinadamu. Yesu ameshatuachia mfano hai nanyi fanyeni hivyo hivyo. Tutumie muda wetu kuweka katika matendo yale aliyotuachia Bwana - nanyi fanyeni hivyo hivyo. Tuinuke, twende tukawaoshe wenzetu miguu, mikono na hata miili yao.

Bwana Yesu katika upendo wake alituona tumechoka, tu wachovu, tulihitaji kuoshwa, kulishwa na kupumzika. Nawe ndugu yangu chukua dakika chache uone leo, dunia yetu inahitaji nini zaidi ya hicho ufanyacho. Jirani yako anahitaji nini zaidi, mwenzako wa ndoa, watoto wako, mtaa wako, jumuiya yako n.k unaahidi nini kwao katika pasaka hii unayoadhimisha mwaka huu? Yesu aliona mahitaji yetu akatupatia maji tunywe na mkate tule ili tubaki wazima daima. Yesu ametupatia ekaristi, daraja la upadre na zaidi sana jukumu la upendo ili tuweze kufika kwake. Na siyo kufika tu bali tufike tukiwa wazima na si wafu. Tunalo jukumu la kutakatifuza hali zetu, maisha yetu  na sadaka zetu zaidi ili tufike mbinguni.Hilo ndilo lengo na mapenzi yake baba.

UFAFANUZI WA KINA

Katika injili, Mtume Petro anasita kuoshwa miguu na Yesu. Baada ya mvutano anakubali. Kuosha na kuoshwa miguu ni sehemu ya maisha ya kikristo. La muhimu zaidi ni kumwacha Yesu atuoshe sisi. Nisipokuosha mimi basi huna shirika nami  - Yoh 13:8. Kwanza Yesu hutuosha miguu sisi ili tuwe safi. Halafu tukishakuwa safi tunapata nguvu na uwezo wa kuosha wengine. Mtume Petro alipoelewa hilo alishinda mashaka yake na akalia Bwana si miguu tu bali hata mikono na miguuu – Yoh. 13:9. Kutoka kwetu Yesu anahitaji uwepo wetu na kumpa Yesu nafasi ya kutuosha miguu. Matokeo yake ni sisi kufanya kama alivyofanya Bwana yaani kuosha  miguu ya wenzetu. Baada ya Bwana kuwaosha miguu aliwaambia mmeelewa nilichofanya? Mwaniita mwalimu na Bwana na ni sawa. Kama mimi nimefanya hivyo basi nanyi fanyeni hivyo kati yenu – Yoh. 13:13-15.

Alikwisha kusema kuwa ni lazima kula mwili wake na kunywa damu yake ili kuupata uzima wa milele. Hivyo ekaristi kuu ya Yesu inaanza kwa kuosha miguu na kumalizika na ushuhuda katika utukufu wa msalaba. Hapa Yesu anaonesha wazi utukufu wa Mungu katika umbo la mwili. Anachukua hali ya mtumwa ili tuweze kumfikia. Yesu anajifunua ili tuweze kuuona utukufu wa Mungu.

 

Yesu anakula pamoja na mitume kama walivyofanya wengine lakini katika mlo huu anaongeza maneno - toeni mle na toeni mnywe - huu ni mwili wangu na kunywa damu yangu. Marafiki wa kweli hukaa pamoja, huufurahia uwepo wao kati yao na si tu kumbukumbu na matukio. Leo hii na wakati huu kwa imani tunashiriki mapenzi haya ya Mungu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Hapa Bwana Yesu anatengeneza mwanzo mpya wa maisha na namna mpya ya kuishi. Kama ekaristi ni mahali ambapo bwana huosha miguu yetu basi maisha ni mahali ambapo sote hatuna budi kuoshana miguu. Ekaristi ni maisha na maisha ni Ekaristi.

 

 Zawadi na mfano tuupatao katika kuosha miguu ni kielelezo tosha cha ukristo wetu. Tusiufananishe ukristo na mtindo fulani wa kimaadili/kimaisha tu. Kwanza ya yote ni zawadi – Mungu anajitoa mwenyewe zawadi kwa ajili yetu. Hatoi kitu bali yeye anajitoa mwenyewe – anakuwa uzima yaani katika Fumbo la  Ekaristi. Tunahitaji kuosha miguu - alama ya unyenyekevu kabisa na Yesu alifanya hivyo akijua aina ya kifo kinachomsubiri - kama mwizi -akafanya hivyo akionesha mfano - kuosha dhambi zetu kila siku. Tutafakari juu ya sakramenti ya kitubio. Katika sakramenti hii daima Yesu anaosha dhambi zetu ili tuweze kukaa meza moja naye. Yesu aliosha miguu wakati wa karamu ya mwisho. Wakristo wa kwanza walielewa ni mlo wa aina gani. Walisherehekea hilo siku za Dominika ikawa mazoea yao.

 

Mazingira ya nchi ya Palestina - milima na mawe. Na safari nyingi wakati ule zilifanywa kwa miguu na msafiri alipofika au kwa mwenyeji au mahali pa kulala alipewa maji ya uvuguvugu ili kukanda na kuosha miguu iliyokuwa imechoka na kudhoofu. Baada ya hapo alipewa chakula na mwenyeji wake. Ikieleweka katika mtazamo huo, Ekaristi ni mahali pa kuponea kwa ajili ya wasafiri. Maisha ya mkristo ulimwenguni ni safari ya hija, safari ndefu. Njiani tunakumbana na mengi, vishawishi na kukata tama. Yesu katupatia Ekaristi mahali pa kuweza kupata nafuu na afadhali ya maisha. Tunapotoa komunyo pamba kwa mgonjwa twaita viaticum - msaada wa safari, hutupatia nguvu katika safari na katika mahangaiko ya maisha.

 

KKK 1409 – EKARISTI NI KUMBUKUMBU YA PASAKA YA KRISTO, yaani ya kazi ya wokovu iliyotekelezwa kwa maisha, kifo na ufufuko wa kristo, kazi inayofanywa iwepo kwa tendo la kiliturjia.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.