2015-04-03 12:05:00

Jenerali Buhari kukichezesha kwata Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram


Ni matumaini ya Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria kwamba, Rais mteule Muhammadu Buhari wa Nigeria, ataweza kusoma alama za nyakati na kuanza kushughulikia matatizo na changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili wananchi wa Nigeria kwa sasa bila kupoteza wakati. Ni jambo la kutia moyo kwamba, Rais anayeng’atuka kutoka madarakani Goodluck Jonathan amekiri hadharani kushindwa katika uchaguzi mkuu, jambo ambalo limemwongezea sifa na heshima miongoni mwa wananchi wa Nigeria na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake.

Hili ni tukio la kihistoria nchini Nigeria, kwani viongozi wengi waliokuwa wanashindwa chaguzi kuu, hawakuwa wanakubali kushindwa kutokana na visingizio kibao ambavyo viliipelekea machafuko ya hali ya hewa nchini humo. Uchaguzi umefanyika katika hali ya utulivu licha ya mashambulizi yaliyofanywa na kikundi cha Boko Haram. Wananchi wa Nigeria wameonesha ukomavu katika siasa kwa kuachana na ukiritimba ulioneshwa na Chama tawala kwa kipindi cha miaka kadhaa, hali ambayo iliwafanya viongozi wengi kulewa na madaraka na hivyo kushindwa kushughulikia mateso na mahangaiko ya wananchi wa Nigeria.

Kardinali Onaiyekan anabainisha kwamba, kwa sasa changamoto kubwa zilizoko mbele yao ni kujenga umoja, udugu na mshikamano wa kitaifa, ambao umesambaratishwa kutokana na mashambulizi ya kikundi cha Boko Haram yanayojikita katika udini. Majadiliano ya kidini, ni changamoto kubwa kwa Rais Buhari ambaye ni mwamini wa dini ya Kiislam, hapa itampasa kuonesha umuhimu wa majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani na kwamba, tofauti za kidini kisiwe ni chanzo cha chokochoko na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia bali ubani wenye harufu nzuri kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.