2015-04-03 08:29:00

Ijumaa kuu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu duniani!


Msalaba ni alama angavu ya upendo wa Mungu unaomlinda na kumkomboa mwanadamu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa pia ni vyombo vya upendo na ulinzi kwa jirani zao. Hivi ndivyo anavyotafakari Askofu mstaafu Renato Corti wa Jimbo Katoliki la Novara, Italia katika Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo, mjini Roma, wakati wa Ijumaa kuu usiku, tarehe 3 Aprili 2015.

Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Mada ambazo zinachambuliwa na kufanyiwa tafakari ya kina ni pamoja na: maendeleo endelevu ya binadamu; vita, madhulumu na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu; familia na changamoto zake; mateso na mahangaiko ya binadamu; dhuluma na nyanyaso dhidi ya watoto wadogo pamoja na utumwa mamboleo, mambo ambayo yanakwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hii ni Njia ya Msalaba inayojitahidi kumwilisha sauti, mawazo na vionjo vya Yesu Kristo, kama anavyobainisha Askofu mstaafu Renato Corti. Tafakari inalenga kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusikiliza kilio cha Yesu Kristo wakati wa Njia ya Msalaba, kuelekea Kalvari. Kila kituo kina ujumbe mahususi kadiri ya mazingira ya watu wa nyakati hizi. Licha binadamu kukengeuka na kumwasi Mwenyezi Mungu, lakini bado upendo huu wa Mungu unaendelea kumlinda mwanadamu kwa kutambua kwamba, upendo huu ni zawadi na unafikia kilele chake pale Mlimani Kalvari.

Kutokana na changamoto hii, kila mtu anahamasishwa kuwa ni mlinzi na mtunzaji wa mazingira na Injili ya Uhai ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kuna maelfu ya watu wanaoendelea kumwaga damu yao kutokana na vita, nyanyaso na madhulumu ya kidini. Kuna maelfu ya watoto ambao wananyanyaswa na kudhalilishwa, wote hawa wanafumbatwa katika Tafakari ya Njia ya Msalaba, tayari kuambatana na Yesu Kristo. Kuna watu wanaoteseka kwa vile tu ni Wakristo au wanasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu.

Watu kama hawa wanaweza kukutana na Yesu anayepelekwa  Mlimani Kalvari kama Kondoo asiyekuwa na mawaa! Kuna watu ambao wana madonda makubwa ya upweke hasi, watu ambao wametengwa na kubaguliwa; wagonjwa na wale wanaokabiliwa na kifo machoni pao. Haya ndiyo mateso na mahangaiko ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili anayeendelea kuchukiwa, kunyanyaswa na kudhulumiwa. Inasikitisha kuona kwamba, askari wasiokuwa na chembe ya huruma wanamvua Yesu nguo zake na kuzipigia kura. Hivi ndivyo inavyoendelea kujitokeza kwa watu wanaodhalilishwa utu na heshima yao kutokana na biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya pamoja na utumwa mamboleo.

Katika Njia ya Msalaba, Yesu anakutana na wanawake wajasiri na mashuhuda wanaoendelea kujisadaka hata leo hii kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria ni mhusika mkuu katika mateso na mahangaiko ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo, anamsindikiza Mwanaye katika Njia ya Msalaba na hatimaye, kumwona akikata roho pale Malimani Kalvari.

Katika mazingira haya, Askofu mstaafu Renato Corti anamdhaminisha Bikira Maria familia na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2015. Baba Mtakatifu Francisko ameyakabidhi maadhimisho haya chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Hata leo hii watu bado wanaendelea kujiuliza, unatoka wapi ukatili na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia? Adhabu ya kifo imepitwa na wakati kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu.

Tafakari ya Njia ya Msalaba ya Askofu mstaafu Renato Corti inatajirishwa na tafakari zilizowahi kufanywa na watu mbali mbali ndani na nje ya Kanisa; watu ambao wamejipambanua kwa kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Tafakari hii inahitimishwa kwa kimya kikuu kinachofunga kinywa cha binadamu kwa kuwaachia wazi moyo wake, ili kukutana na mateso yanayokomboa. Ni mchakato unaomwezesha mwamini kuwa huru kutokana na upendo unaowashikirisha wote pasi na ubaguzi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.