2015-04-02 15:43:00

Utajiri unaofumbatwa katika Kesha la Pasaka


Ninakuleteeni furaha ya Pasaka kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu. Kesha la Pasaka yaani Jumamosi kuu ni Usiku mtakatifu ambapo Kristo mshindaji amejipatia taji kwa kuyashinda mauti. Ni siku ambayo Kristu hayumo tena kaburini bali yu mzima na kwa maana hiyo Kanisa popote duniani linashangilia na kuimba aleluya. Katika litrujia ya usiku mtakatifu Kanisa laelezea jinsi ambavyo Kristu ni Nuru, linaimba sifa za nuru hii kwa njia ya Mbiu ya Pasaka. Kanisa linashangilia ushindi toka upotevu wa mwanadamu na kuelekea uhuru kamili unaoletwa na Kristu mfufuka.

Liturujia ya Jumamosi Kuu imegawanyika sehemu kuu nne, yaani Liturujia ya Mwanga, Liturujia ya Neno, Liturujia ya ubatizo na Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Katika sehemu hizi kuu nne Mama Kanisa ataka tuelewe polepole jinsi historia ya Ukombozi inayopata utimilifu wake kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo.

Katika Liturujia ya Mwanga kawaida tunaanza na ishara ya moto ambao huleta joto na mwanga, hufukuza baridi na giza. Moto unaowaka huonesha uwepo wa Mungu katikati yetu. Alama hii tunaiona pale Wana wa Israeli walipokuwa wakitoka Misri waliongozwa na moto katika wingu. Katika Agano jipya tunaona ndimi na miali ya moto siku ya Pentekoste na hivi Roho Mtakatifu alitua kwa kila mmoja wa Mitume waliokuwa pamoja na Bikira Maria.

Moto ni alama ya utakaso toka uovu na kuelekea utakatifu au wajibu wa kitume, hebu kumbukeni jinsi Nabii Isaya alivyowekewa kaa la moto kinywani mwake na hivi akatangaziwa utakaso wa roho tayari kwa kazi ya kinabii. Isa. 6:6-7. Katika Liturujia ya Kanisa kwa sasa, moto ubarikiwa ili uwe ishara ya upendo na maelewano katika familia, ishara ya kufukuza giza yaani shetani katika maisha ya kikristu. Kumbe tunapowasha Mshumaa wa Pasaka na mishumaa yetu mingine toka moto huu tunataka kumwahidi Bwana zawadi nzuri ya upendo, utayari, heshima tutakayomrudishia sisi wenyewe. Kwa ujumla mshumaa ni uwepo wa Mungu katikakati ya mataifa, katikati yetu na tunasema ni Mungu milele. Angalia taa ya milele kanisani ashilio la uwepo wa Mungu katika Ekaristi takatifu daima katikati yetu.

Maandamano toka moto wa Pasaka hadi kuimbwa Mbiu ya Pasaka SIFA KWA MSHUMAA ishara ya Kristo humaanisha kuwa kanisa linatoa sifa kwa Mwanga mtakatifu ndiye Kristu mfufuka. Mshumaa wa Pasaka katika Litrujia ya ubatizo utatumbukizwa mara tatu, iliyo ishara ya Utatu Mtakatifu kwa maana ya kuyaweka wakfu maji katika Utatu Mtakatifu na kwa njia hiyo mwovu hufukuzwa ili watakaobatizwa katika kisima hicho wapate nguvu ya Utatu Mtakatifu wapate ondoleo la dhambi na kuokolewa toka mauti.

Mpendwa mwanapasaka, baada ya Liturujia ya mwanga huanza Liturujia ya Neno la Mungu ambamo kanisa hutafakari historia ya mwanadamu tangu kuumbwa kwake hadi anapokuja mkombozi na kumalizia na Ufufuko kilele cha mapendo ya Mungu kwa mwanadamu. Katika somo la kwanza tunaona Mungu anaumba kila kitu na anaona ni chema kabisa. Kisha Mama kanisa anatuwekea mbele yetu Ibrahimu Baba wa imani katika somo la pili. Matunda ya imani ya Ibrahimu ni uzao, baraka tele na wokovu. Mwaliko kwetu ni kumsifu Mungu kwa kutuumba na kuomba kujaliwa imani kama ya Ibrahimu.

Katika somo la tatu toka kitabu cha kutoka tunapata kugundua maongozi ya Mungu na upendo wake kwa wanadamu. Anawatoa Misri na anawavusha bahari na mto ishara ya ubatizo, yaani kuzamishwa na kuibuka kuelekea ng’ambo ya pili ulioushindi na utakatifu. Katika somo la Waraka kwa Warumi ujumbe wa mahsusi ni kuwa kuishi kwetu ni Kristo, kwa maana tulikufa naye katika mauti na kufufuka naye katika ubatizo. Sasa tuko wapya na hivi mwaliko ni kuacha dhambi na kuendelea na maisha mapya.

Katika Injili Habari ya ufufuko na ushindi dhidi ya mauti ndiyo imetanda na kupamba kila aina ya adhimisho la Pasaka. Tunaona akina mama ambao Bwana ameamua kuwatuza wao kwanza zawadi ya Ufufuko ikiwa pia ni ishara ya kuinuliwa kwao toka ukiritimba wa kiyahudi. Wanaenda kaburini alfajiri na mapema. Wakiwa na mashaka juu ya nani atawaondolea jiwe juu ya kaburi, wanakuta jiwe halipo! Jiwe ni alama ya kandamizo na hivi kutokuwepo ni kwamba Bwana ni mshindi amelitupilia mbali, ametupilia mbali dhambi, haina nguvu tena juu ya mwanadamu.

Wanamwona kijana mwenye mavazi meupe na anawapa taarifa kuwa Bwana hayupo amefufuka kumbe waende wakaseme kwa wanafunzi wake kuwa awatangulia Galilaya kama alivyokuwa amewaambia. Kijana mwenye vazi jeupe ni alama ya malaika anayetangaza kuwa Kristu ni wa juu na hivi ni mtakatifu na mzima. Taarifa ya kwamba nendeni Galilaya ina maana kubwa sana ya kwamba wasibaki alipofia bali wafikirie Ufufuko na wakaende kwenye jumuiya ya watu si kaburini. Ni mwanzo wa umisionari, ni mwanzo wa msingi wa maisha ya mapendo ya kichungaji kwa jumuiya ya watu.

Neno la Mungu ni taa ya kutuongoza na daima kama tangazo la imani huita na kuzaa matunda ndiyo ubatizo. Kumbe baada ya Liturujia ya Neno hufuata Liturujia ya ubatizo ambamo Mama kanisa hupata watoto wapya. Kisima cha ubatizo hubarikiwa kwa Mshumaa wa Pasaka na hivi nguvu ya Utatu Mtakatifu kwa ajili ya wabatizwa huwekwa na Kristu mwenyewe aliye nuru na mwanga kwa wote. Kisima cha ubatizo hugeuka kuwa tumbo la uzazi kama mama, huzaa watoto taifa teule la kikuhani, kifalme na kinabii. Kwa njia ya ubatizo mtu huifia dhambi na kuacha mambo ya kale na kuingia maisha mapya. Ubatizo ni kielelezo msingi na hasa ndiyo ufufuko. Wale waliokwisha batizwa zamani wanaalikwa katika Liturujia ya ubatizo kurudia ahadi zao za ubatizo na kusonga mbele katika Ufufuko. Na kwa jinsi hiyo Kanisa linakua na kuongezeka ishara ya ushindi dhidi ya shetani.

Mwishoni, Mama kanisa huadhimisha litrujia ya Ekaristi takatifu ambamo sasa waamini wapya hushirikishwa kwanza ukamilifu wa sakramenti za kuingizwa katika ukristu. Hushiriki meza ya mapendo ya Kristo kwa mwanadamu. Hujipatia uzima wa milele kama tufahamuvyo toka Injili ya kuwa aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu ataishi milele. Waamini wote hushiriki matunda ya Pasaka Ekaristi Takatifu. Ni sadaka ya Kristo Msalabani iliyo hai katika Ufufuko. Ekaristi ni chanzo, kilele na chimbuko la umoja wa Kanisa na hivi wote waliofamilia moja wanashiriki mkate mmoja wa mbinguni.

Mpendwa, nikutakieni heri na baraka tele za Mungu katika sherehe za Pasaka ukakirimiwe yote mema sasa na daima na milele.

Tumsifu Yesu Kristo

Tafakari imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.