2015-04-02 09:14:00

Uchaguzi umepita, matokeo yametangazwa, watu wanataka amani na utulivu


Tume huru ya uchaguzi nchini Nigeria imemtangaza Jenerali mstaafu Muhammadu Buhari kuwa mshindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Nigeria, hivi karibuni kwa kupata kura millioni 15.4 na hivyo kumshinda mpinzani wake wa karibu Rais anayemaliza muda wake Goodluck Jonathan aliyepata kura millioni 13. 3. Askofu mkuu Ignatius Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwa makini wakati huu ili kulinda na kudumisha amani, utulivu na usalama wa raia na mali zao dhidi ya mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa Barani Afrika wamempongeza Rais anayemaliza muda wake Goodluck Jonathan kwa kukubali kushindwa na kumpongeza Rais mteule Buhari, jambo linaloonesha moyo wa uzalendo unaopania kudumisha mchakato wa demokrasia ya kweli katika ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi. Amewashukuru wananchi wa Nigeria waliompatia dhamana ya kuwaongoza na kwamba, ataendelea kuchangia ustawi na maendeleo ya taifa la Nigeria anayetarajiwa kukabidhi madaraka mwezi Mei, 2015 jadiri ya Katiba ya nchi.

Rais mteule Buhari amempongeza Bwana Goodluck Jonathan kwa kutambua na kuthamini utashi wa wananchi wa Nigeria waliouonesha kwa njia ya kura na hivyo kusaidia mchakato wa mabadiliko katika uongozi wa nchi kwa njia ya amani. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Nigeria, kiongozi aliyeshindwa katika uchaguzi mkuu anakiri mara moja bila ya kigugumizi. Viongozi hawa wawili wamekubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi li kuhakikisha kwamba, kipindi hiki cha mpito kinatawalia na amani na utulivu, ili kurejesha tena utawala wa sheria na wala si baadhi ya watu kujichukulia sheria mikononi. 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.