2015-04-02 11:53:00

Kardinali Parolin: Uchumi na fedha ni vyombo vya maendeleo ya binadamu


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahamasisha wanasiasa, wachumi, waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao barabara kama sehemu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayojikita katika  utekelezaji makini wa dhamana na majukumu katika medani mbali mbali za maisha.

Sera na mikakati mbali mbali ya kisiasa na kiuchumi haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa huduma makini kwa utu na heshima ya binadamu na kamwe fedha isimgeuze mwanadamu kuwa mtumwa. Uchumi uwaangalie na kuwahudumia maskini, wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwa njia hii, uchum unakuwa  ni nyenzo msingi katika ukuaji wa mtu, jamii na nchi katika ujumla wake.

Ni mchango wa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alioutoa wakati akichangia mada kwenye Kongamano lililokuwa linajadili kuhusu fedha na masuala ya kisiasa mjini Roma. Anasema, uchumi hauna budi kuwa ni chombo cha huduma kwa binadamu na wala si mtawala na mnyanyasaji. Serikali na taasisi za masuala ya uchumi na fedha hazina budi kuzingatia: sheria na kanuni maadili katika upangaji wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawajali na kuwashirikisha hata maskini katika kupanga na kutekeleza mikakati ya uchumi na maendeleo inayowagusa kwa karibu zaidi, ili kweli uchumi uweze kuendana na mahitaji msingi ya binadamu.

Kardinali Parolin anasema, kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 11 Aprili 2015 kwa mara ya kwanza Nchi ya Cuba itashiriki katika mkutano wa nchi za Amerika utakaofanyika mjini Panama, changamoto na mwaliko wa kuweka msingi thabiti wa ushirikiano na mfungamano wa Jumuiya ya Kimataifa. Ni fursa ya kuangalia changamoto zilizopo hasa kuhusiana na wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na ubora wa maisha nchini Marekani.

Katika kongamano hili, Bwana Pietro Grasso, Rais wa Seneti ya Italia ameshiriki kwa kuwahimiza wanasiasa na serikali katika ujumla wake kusimama kidete katika kushughulikia kwa umakini mkubwa changamoto mbali mbali zinazoibuliwa katika masuala ya uchumi na fedha, ili kweli mwanadamu aweze kuhudumiwa kikamilifu, kwa kukidhi mahitaji msingi ya binadamu. Kwa sasa uchumi na fedha ni mambo mawili yanayokinzana na athari zake zinawangukia raia wa kawaida.

Kuna ubadhirifu mkubwa wa uchumi na shughuli zinazofanywa kinyume cha sheria; mambo ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa fursa za ajira. Kuna kiasi kikubwa cha fedha ambacho kiko mikononi mwa wananchi, lakini hakijulikani na Benki kuu. Yote haya ni mambo ambayo yanachangia wasi wasi pamoja na mwendelezo wa athari za myumbo wa uchumi kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.