2015-04-02 08:28:00

Fumbo la Msalaba na upendo wa Mungu!


Leo, Kanisa linapenda kuungana na wote wanaoelemewa na Msalaba kwa kutafakari kuhusu Kashfa ya Msalaba na utukufu wa Mungu! Marko 15:1-39. Kazi kwako! Waziri mmoja akiwa katika mkutano mkuu wa Bunge la nchi alipolaumiwa na kumtishia na baadhi ya wabunge kuenguliwa uwaziri aliinuka kitini kwa ujasiri wote na kusema: “Nitafurahi sana kuondolewa madarakani kwa kuwa kazi ninayoifanya ni sawa na kubeba Msalaba mzito.” Tamko kama hilo utawasikia wanalitoa wanaoteseka kwa kazi nzito, wanaoteseka kwa magonjwa mbalimbali, wenye maisha magumu, wanaodhulumiwa, wanaoteseka na kusumbuka kwa namna moja au nyingine wanalalamika: “mwenzenu ninao Msalaba, au mwenzenu nimebeba Msalaba mzito wa maisha, au  mwenzenu ninakufa.”

 

Mateso na masumbuko hayo yanaweza kuwa ya jamii au jumuia fulani kwa pamoja: Kwa mfano iliwatokea wayahudi pale manabii wao walipowaonya na kuwatahadharisha, “ jamani msitende dhambi, vinginevyo mtaenda utumwani”, watu walipoacha kutikia mwito wa manabii, wayahudi wote pamoja na manabii wao wakasombwa kwenda utumwani. Huko utumwani wote kwa pamoja bila kumwacha Nabii wakateswa na kufanyishwa kazi nzito za kitumwa. Hivyo ndivyo ilivyo taratibu ya misalaba.

 

Kadhalika siku za leo yawezekana taifa fulani likayumba kiuongozi na kukosekana sauti ya kinabii inayoweza kusikika, kwa sababu ya sauti ya kiongozi wa serikali inakosa busara na mwelekeo, kadhalika inatokea lugha ya viongozi wa dini inabaki kutoa milio inayogongana. Unaona waziwazi nchi inaingia katika giza totoro na kuwa  “hoovyo kama mji usio na jumbe.” Hapo utamsikia hata raia mjinga anaongea lake: “Viongozi wetu ni Msalaba mtupu!”  au waswahili watasema, “tunao viongozi bomu” na bomu likikulipukia mapato ni mateso na kifo kwa taifa zima bila kujali kiongozi au mwongozwa. Kama wananchi ni msalaba kwa viongozi na viongozi ni msalaba kwa wananchi, hapo ujue raia wote na viongozi wao ni misalaba mitupu! Hii ndiyo sera ya Msalaba. Kwa hiyo endapo mateso ni Msalaba, basi kila binadamu amebeba Msalaba wake.

 

Mateso na misalaba hiyo imekuwa tangu kuumbwa kwa Adam na Eva. Katika kila nyakati za historia binadamu amebeba msalaba ana daima amejaribu kwa juhudi zake zote za binadafsi hata kijumuia kuutua msalaba huo, lakini ameshindwa. Mapambano ya kuukataa msalaba yanaendelea wakati huo huo misalaba mipya inaibuka kila wakati. Katika hali kama hiyo kunakuwa na baadhi ya watu wanaoamua kuyapokea mateso wakijituliza na kusema: “Likikupata patana lalo.” Kwa hoja hiyo, wengine wameamua kuyatengenezea ishara hayo mateso yaani kuchonga msalaba wa mti na kuusujudu. Wameutundika msalaba huo kwenye nyumba zao za ibada hata majumbani mwao, nao umesimama kama bendera inayoairisha ushindi duniani. Watu hao hawakomi tu katika kuutundika juu ya minara ya kanisa bali wanapiga ishara ya msalaba wakati wa sala, ingawaje kuna badhi yao wakiwa mbele ya watu wanajishauri kupiga ishara ya msalaba waziwazi. Wengine wanauvaa shingoni, wengine vidoleni, nk.

 

Wakristo wa Kikoptiki huko Misri na Ethiopia huchora (tatoo) Msalaba usiofutika kwenye kiganga cha mkono au kwenye panda la uso ili kuhalalisha mateso aliyo nayo mtu. Siku hizi hata wakoptiki wale wasiofanya tatoo wanavaa msalaba shingoni. Kuna baadhi ya Madhehebu ya Kikatoliki huko Kanisa la Mashariki, Padre mwongoza misa daima anashika msalaba mdogo mkono wa kulia anaoutumia kwa kubariki. Ijumaa kuu Wakristo wanauabudu Msalaba kama Mungu. Kulikoni?

 

Ndugu zangu msalaba ulio ishara ya mateso na kifo, unamwakilisha Kristu ambaye ni Mungu mwenyewe. Mungu anaainishwa kuwa ni upendo. Kwa hiyo kama Mungu ni Upendo, nao upendo umejidhihirika katika Yesu aliyeteswa na kufa msalaba kwa ajili ya kutupenda. Kwa hoja hiyo mkristu anapouona msalaba mara moja anakumbuka upendo wa Mungu. Mkristo anapouona msalaba anamshukuru Mungu, kwa kuwezeshwa kuelewa maana ya mateso. Ama kweli msalaba ni fumbo la upendo wa Mungu kwa binadamu.

 

Kwa maana hiyo, wakristu wametenga juma moja kamili kati ya majuma hamsini na mbili ya mwaka mzima wakiliita, “Juma kuu, Juma la mateso, Juma takatifu.” Katika juma hilo wakristu wanatafakari mateso na kifo cha binadamu, yaani mstakabali wa maisha yetu. Kwa kufanya hivyo hatukumbushwi tu mateso ya Yesu, bali tunashirikishwa kikamilifu kuyaishi mateso ya Kristo na mateso yetu pia. Kama tunasadiki kuwa Kristu yuko ndani ya kila mtu, na tukijua kuwa sisi sote tunafanya mwili wa Kristu, hapo basi tunaweza kuonja na kushiriki kikamilifu kuwa Kristo yuko bado hadi leo anateseka na yuko katika machungu mazito na katika kifo hadi mwisho. Tunalionja hilo waziwazi kwamba yuko bado amesulibiwa katika ndugu zetu wote wanaouawa kwa bunduki na mabomu sehemu mbalimbali nchini mwetu, Yesu yuko kwa wanaouawa kwa ajali mbalimbali mabarabarani, majini, wanaoonewa majumbani, makazini, wanaodhulumiwa na viongozi, nk.

 

Yesu yumo katika wale wanaoteseka na kuzurura mitaani na vijijini, kwa wale wanaoteseka kwa kukosa makao, au chakula nk. Kwa hiyo tunajisikia kuishi wakati uleule wa mateso ya Mungu na katika watu na tunaweza kushiriki kama wamama wale waliosimama chini ya msalaba wa Kristu pale Kalvarini. Tuko karibu ya misalaba isiyo na mwisho ya ndugu zetu mbalimbali. Basi tuubusu msalaba wa Kristu katika ndugu zetu, kama walivyofanya watakatifu wote. Ama kweli sisi tunao msalaba na tunakuwa watu wa wakati uleule wa Msalaba wa Yesu.

 

Mungu huyo alipokuwa msalabani aliambiwa: “Aliwaokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.” Hivyo ndivyo alivyo Mungu. Hafikirii kujiokoa mwenyewe. Anajitoa na kujiaminisha kabisa, na kujiacha kwa ajili ya upendo. Picha ya kale ya Mungu budi ibomolewe kwani Mungu hataki sadaka nyingine yoyote ile kwa sababu anajisadaka mwenyewe. Ufurahi ewe mkristu, kwa vile baada ya miaka elfu mbili baada ya Kristo, sisi tuko bado ngangali kama wale wamama waliosimama chini ya msalaba, au kama mitume, na kama yule Jemedari (askari) tumesimama tukishangaa, tukistaajabu, tukiupenda Msalaba. Tunafahamu kwamba katika msalaba kuna uzuri, kuna mvuto, kuna ukweli wa maisha, kuna upendo. Msingi wa imani ya kikristu katika msalaba ni kitu kizuri kupita kila kitu hapa duniani, kwani msingi huo umejengwa katika upendo.

 

Msalaba huo uliosimikwa duniani umechomoka kuelekea mbingu, msalaba huo ndiyo unaowakokota binadamu wote kuelekea mbinguni. Mtu anazaliwa toka kwenye moyo wa upendo wa Mungu mwumbaji usiolindwa. Ama kweli upendo hauna mlinzi. Huwezi kuulinda upendo nao hauwezi kujitetea huo ndiyo msalaba. “Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake; Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

 

Lakini kumbe Mungu hakuwa amemwacha mwanaye. Mungu hatuokoi kutoka msalaba, bali anatuokoa katika msalaba; Mungu hatulindi kutoka kwenye maumivu na machungu, bali anatulinda katika maumivu na uchungu. Ndiyo maana zaburi ile ya uchungu – “Mungu wangu, Mungu wangu” – ambayo Yesu anaisali inaishia kwa tamko hili: “Ee Bwana umenijibu, umenihuisha.” Kuimarisha huko maana yake siyo kuniepusha na mauti, la hasha bali kunivusha na kunihuisha, kunipa moyo.

 

Upendo unawajibu mwingi sana, lakini wajibu mmoja wapo na wa maana zaidi ni ule wa kuwepo pamoja na kile unachokipenda. Mungu yuko msalabani kusudi awe kama mimi na awe pamoja na mimi, ili mimi niwe naye na pamoja naye. Mtu wa kwanza na wa pekee kuonesha tendo la imani siyo mwanafunzi wa Yesu bali ni mgeni, yaani yule akida askari shujaa wa kirumi ndiye anayeshuhudia ushuhudia ushujaa wa askari wa kweli. Ndivyo anavyoandika Mwinjili Marko: “Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.” Unaona Yesu (Shujaa mkuu) hatoi mwanga wa pekee, wala haoneshi kaburi wazi, la hasha bali katika giza la mateso ya Ijumaa kuu, na kwa kuona mateso makuu ya Msalaba, na katika kiti cha dhihaka (Msalaba) ndipo yule askari aliye mahiri wa kuua, aliyeshuhudia na kuwaua watu zaidi ya mia moja, anathubutu kusema: “Mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”

 

Maana yake, kufa namna hii, kifo cha upendo, hilo peke yake inatosha kuwa ni ufunuo na ni jambo la Mungu. Shujaa ameona katika Yesu, kitu tofauti na kinyume kabisa na anachoweza kufanya askari wa kawaida.  Askari huyu Mrumi anajua kwamba ukuu wote ni kwa wale walio wakuu, wale katiri na wauaji wakuu. Kinyume chake, kumbe, juu ya Msalaba unaona ukuu na mamlaka ya Mungu, kwamba msalaba hauhifadhi kifo bali utoa maisha. Upendo siyo kutawala bali kutumikia. Ama kweli mateso ni kitendawili au Fumbo la upendo.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.