2015-04-01 11:04:00

Waamini walei ni "majembe" ya nguvu katika mchakato wa Uinjilishaji


Waamini walei wanapaswa kuwa ni uti wa mgongo katika mchakato wa Uinjilishaji, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Mtakatifu Paulo anawakumbusha Wakristo kwamba, katika maisha yake, alivipiga vita vikuu, imani akailinda. Huu ni mwaliko pia kwa Wakristo wa nyakati hizi kupambana kufa na kupona, ili kulinda, kutetea na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Waamini wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba wanao mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Waamini wawezeshwe kwa kupewa majiundo makini na endelevu ili waweze kushiriki vyema katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wao ni Familia ya Mungu inayowajibika, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya kwanza ya Maaskofu Barani Afrika.

Haya ndiyo yaliyoibuliwa hivi karibuni wakati wa mkutano mkuu wa Halmashauri walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso, uliohitimishwa hivi karibuni kwa kuwashirikisha wajumbe kutoka katika Majimbo 15 yanayounda Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso.

Waamini walei wanapaswa kufundwa, kukua na kukomaa, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa,  Familia ya Mungu inayowajibika. Waamini walei wanaowajibika ni nyenzo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa na wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Kwa njia ya sakramenti ya Ubatizo, waamini walei wanaendeleza maisha na utume wa Kanisa katika maeneo yao, huku wakitambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika.

Mama Bernadette Konfè, Mwenyekiti wa Halmashauri Walei, Taifa anasema, hii ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji inayopania kuwahamasisha waamini walei kuhakikisha kwamba, wanajisikia kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu inayowajibika katika kila hatua ya maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso limeaandaa kikosi kazi cha wajumbe 55 watakaotoa mafunzo ya awali na endelevu kwa ngazi ya kitaifa na kundi la watu 15 watakaoendesha mafunzo katika ngazi ya Kijimbo.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, mikakati na maamuzi yaliyofikiwa kwenye Mkutano mkuu wa Halmashauri Walei yanawafikia waamini walei Majimboni na Parokiani, ili waweze kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.