2015-04-01 10:18:00

Padre ni mchungaji, mfuasi na kiongozi wa Watu wa Mungu


Tasaufi ya maisha ya kipadre mintarafu maelekezo ya Baba Mtakatifu Francisko ni mada ambayo imefafanuliwa hivi karibuni na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Wakleri wakati alipokuwa natoa mada kwenye kongamano kuhusu tasaufi ya kipadre. Baba Mtakatifu Francisko anasema Padre anapaswa kuwa ni mfuasi amini wa Kristo anayebeba ndani mwake dhamana kubwa mintarafu maisha na utume wake kwa Familia ya Mungu.

Padre kama mfuasi wa Kristo lazima atajibidisha kuhakikisha kwamba, anajenga na kuimarisha mahusiano mema na Yesu Kristo, Bwana na Mwalimu kwa njia ya: Sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti. Ni kiongozi anayetambua kwamba, maisha yake ni hija endelevu inayomwajibisha kushikamana na Yesu daima, ili kufikiri na kutenda kadiri ya Yesu anavyomtaka. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Mapadre watambue kwamba wao ni wachungaji na kamwe si wafanyakazi wala wafabiashara. Familia ya Mungu imtambue Padre kutokana na ushuhuda wa maisha na utume wake.

Padre ni kiongozi wa Familia ya Mungu anayewajibika kikamilifu kwa watu aliokabidhiwa kwake na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anawasaidia kuwapeleka kwa Yesu Kristo. Anapaswa kuwa na fadhila za kibaba na wala si “Meneja” katika shamba la Bwana. Padre ahakikishe kwamba, anatumia vyema madaraka, ili kulinda na kudumisha upendo wa Mungu ambao umehifadhiwa katika moyo wa mwanadamu. Padre kamwe asitumie madaraka yake kuwakomoa watu!

Padre anapaswa kuwa ni kiongozi anayeandamana na watu wake katika furaha na majonzi, anayewatambua watu wake kwa majina na daima yuko kati ya watu wake kama ndugu na wala si mfadhili. Awe ni mhudumu mwaminifu anayejisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu, kwa kuwatangazia na kushuhudia sura ya Kristo Mkombozi wa ulimwengu.

Padre anapaswa kuwa ni kiongozi na nabii. Kardinali Stella anasema, hadi hapa anaendelea kupembua sifa na karama za Padre, kadiri ya changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi, hotuba, nyaraka, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Mapadre watambue fursa, matatizo na changamoto kubwa zilizoko mbele yao, ili wasimezwe na malimwengu na kujikuta kwamba, wako nje kabisa na maisha pamoja na utume wao. Watu wa Mungu wanapaswa kuwa daima na mchungaji mintarafu Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwakumbusha Wakleri kwamba, wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa na Jamii inayowazunguka na wanapaswa kutenda kama wachungaji wema na watakatifu. Zawadi ya Daraja Takatifu inapaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kwa furaha na udumifu, ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Padre anapaswa kuendelea kutambua kwamba, yeye ni mfuasi wa Kristo, dhamana endelevu katika maisha na utume wake; anapaswa kumkimbilia Kristo ili aweze kumganga na kumponya kutokana na udhaifu na mapungufu  yake ya kibinadamu. Padre anaweza kuteleza na kuanguka, lakini awe na ujasiri wa kusimama na kuendelea na safari ya maisha na utume wake.

Padre ni mchungaji anayetumwa na Kristo kuinjilisha kwa njia ya mfano wa maisha na utume wake, ni mhudumu wa Mafumbo Matakatifu ya Kanisa, anayewashirikisha Watu wa Mungu Injili ya Furaha na Matumaini. Padre anapaswa kuwa mtii mbele ya Mwenyezi Mungu na Kanisa, ili kulinda na kuendeleza wito, maisha na utume wake, kwa kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu pamoja na watu aliokabidhiwa na Mama Kanisa. Padre atambue kwamba, ni mchungaji na mfuasi wa Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.