2015-04-01 11:33:00

Lindeni wananchi wa Syria dhidi ya mauaji, dhuluma na ukatili!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linabainisha kwamba, katika kipindi cha miaka minne ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria zaidi ya watu 220, 000 wamefariki dunia, watu millioni 7 hawana makazi maalum na kwamba, wanahitaji msaada wa dharura kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa huko Syria. Umoja wa Mataifa unasema kwamba, hii ni kati ya changamoto kubwa kuwahi kutokea katika Karne ya 21.

Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linaitaka Serikali ya Canada kusaidia mchakato utaoiwezesha Jumuiya ya Kimataifa, kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za wananchi wa Syria. Vita, nyanyaso na madhulumu yanayoendelea huko Mashariki ya Kati, yanawafanya wananchi zaidi ya millioni 4 kutafuta hifadi ya maisha katika nchi za Lebanon, Uturuki na Yordani na kati yao kuna watoto millioni 1. 7, ambao maisha yao yako hatarini.

Vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati inaathari kubwa katika shughuli za kiuchumi, kijamii, kisiasa, kidini na kitamaduni. Kuna changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za kijamii kwa waathirika na wananchi wanaoishi katika nchi husika, ikizingatiwa pia na uhaba wa rasilimali fedha na watu kuwa ni haba na finyu kabisa.

Mataifa yanayoendelea kutoa hifadhi hayawezi kuchukua dhamana kubwa kiasi hiki ya kuwakaribisha, kuwahudumia na kuwalinda wahamiaji na wakimbizi bila msada na mchango kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa. Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Canada inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, vita huko Mashariki ya kati vinakoma kwa njia ya diplomasia na watu wanarudia katika hali yao ya kawaida.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.