2015-04-01 14:14:00

Fursa za ajira ziwekwe kwenye mipango mikakati ya maendeleo endelevu


Kuna Umuhimu mkubwa wa kuweka suala la Ajira katika ajenda ya maendeleo, mipango na progamu ya Mataifa yote duniani. Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema hayo tarehe 30 Machi, 2015 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York wakati wa ufunguzi wa Mkutano unaozungumzia jinsi ya kupata Maendeleo endelevu kwa kukuza ajira na kazi zenye utu

Rais Kikwete amesema tatizo la ajira lina pande mbili, kwanza linaweza kutumika vizuri pale wawekezaji wanapokuja barani Afrika, wanaweza kupata nguvu kazi iliyopo tayari, ikiwa inakidhi matakwa ya kazi na pili ni changamoto kubwa pale ambapo ajira hazipatikani kwa kundi kubwa la vijana ambao wanaongezeka kila mwaka.

"Hivyo ni muhimu ukuzaji wa ajira kuwa kipengele muhimu katika ajenda ya maendeleo, mipango na programu mbalimbali katika Mataifa yote"Rais amesema na kuelezea kuwa pamoja na ukweli uliopo kuwa nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Tanzania, zimeonyesha hali nzuri ya uchumi kwa miongo miwili mpaka mitatu iliyopita, na kuonyesha kuwa bara la Afrika ni moja ya mabara yanayokua kwa kasi kiuchumi duniani, bado bara linakabiliwa na tatizo kubwa la ajira.

"Natarajia tutabadilishana mawazo ya jinsi gani Afrika inaweza kutatua tatizo hili na pia kupata mawazo ya nini kifanyike kuweza kuvutia wawekezaji zaidi". Rais amesema.  "Pia nitapenda kupata mawazo na ikiwezekana kuunga mkono katika kusaidia vijana wetu katika suala la kujiajiri" ameongeza na kusema suala hili linahitaji programu maalum na miradi.

Rais Kikwete amezungumzia suala la ajira barani Afrika kuwa la kutia mashaka na hivyo kuhitaji hatua za haraka. Takwimu zinaonesha kuwa Afrika ilitengeneza ajira 37 million pekee kwa kipindi cha muongo uliopita, kati ya hizi asilimia 28 zilikuwa ajira zenye utu, na wakati huo huo inakadiriwa kuwa, soko la ajira barani Afrika linapokea watu milioni 122 katika ajira mpya kila mwaka.

"Hii inatisha sana kwa vile karibu watu 200 barani Afrika ni wake wenye miaka 15 na 24 na kwamba idadi hii itaongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2045"  Rais amefafanua na kuonyesha wasiwasi wake kwamba bara la Afrika litakumbwa na idadi kubwa ya ukosefu wa ajira, na kibaya zaidi idadi kubwa kuwa ya vijana.


 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.