2015-03-31 11:36:00

Nigeria uchaguzi umekwisha, kimbembe sasa ni matokeo!


Uchaguzi mkuu nchini Nigeria umefanyika na kumalizika, licha ya wasi wasi, vitisho na mashambulizi ya kikundi cha kigaidi cha Boko Haram. Wananchi wanataka kuona mageuzi katika masuala ya kisiasa, kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, utulivu na maridhiano, vikolezo muhimu sana vya maendeleo na ustawi wa jamii yoyote ile. Wananchi wanasema wamechoka kuona damu ya watu wasiokuwa na hatia ikimwagika kila kukicha kana kwamba, hakuna Serikali iliyopewa dhamana ya kulinda na kutetea raia na mali zao.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon alikuwa ameitaka Serikali ya Nigeria kuhakikisha kwamba, inafanya uchaguzi katika mazingira ya amani na utulivu, lakini kwa bahati mbaya, taarifa zinaonesha kwamba, zaidi ya watu 50 wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Boko Haram.

Askofu Oliver Dashe Doeme wa Jimbo Katoliki Maiduguri anasema, uchaguzi mkuu Jimboni mwake umefanyika katika mazingira ya amani na utulivu, ingawa kuna baadhi ya maeneo ambayo yametikiswa kwa mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Boko Haram, kiasi cha kulazimika kuendelea na uchaguzi mkuu siku iliyofuata, yaani Jumapili tarehe 29 Machi 2015. 

Tatizo kubwa lililojitokeza na vifaa vya uchaguzi kushindwa kutambua alama za vidole za wapiga kura. Wananchi wengi wa Nigeria anasema Askofu Doeme wana matumaini makubwa ya kuona mabadiliko yakijitokeza wakati huu baada ya zoezi la kuhesabu na kutangaza washindi kukamilika. Kwa hakika anasema Askofu Doeme hizi ni cheche za matumaini nchini Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.