2015-03-31 09:32:00

Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi: Haki, amani, utu na heshima ya watu


Maadhimisho ya Jumapili ya Matawi huko Mashariki ya Kati yamefanyika kwa kishindo huku viongozi mbali mbali wa Kanisa wakizungumzia kuhusu mauaji ya kikatili, nyanyaso na dhuluma za kidini dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto na mwaliko wanasema viongozi wa Kanisa huko Mashariki kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, kwa kumwomba Bwana wa amani aweze kuujalia ulimwengu haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kipindi cha Juma kuu, ni mwaliko kwa waamini na wapenda amani sehemu mbali mbali za dunia, kuendelea kuchuchumilia: misingi ya amani, majadiliano na upatanisho na maridhiano kati ya watu, changamoto kubwa inayotolewa na viongozi wa Kanisa huko Mashariki ya Kati. Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu ameadhimisha Ibada ya Jumapili ya Matawi kwenye Mlima wa Mizeituni. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa Wakristo kutoka Israeli na Palestina, kuonesha mbegu ya matumaini kwa Wakristo wanaoishi katika Nchi Takatifu.

Askofu mkuu Paul Youssef  Matar wa Jimbo kuu la Beirut, Lebanon katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa watu kujipatanisha na nafasi zao, na kati yao na Mwenyezi Mungu, ili kujenga misingi ya haki, amani na mardhiano kati ya watu mbali na vita, kinzani, dhuluma na nyanyaso mbali mbali. Haki msingi za watu, heshima na utu wao ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya maendeleo ya kijamii.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaendelea kuhamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha umoja, mshikamano na mustakabali wa wananchi wa Lebanon, kwa ajili ya mafao ya wengi. Wananchi waendelee kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Wakristo wanakumbushwa kwamba, hakuna sababu ya kukimbia nchi na urithi kutoka kwa wazazi wao, jambo la msingi ni kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, haki msingi za wananchi zinalindwa na kuheshimiwa.

Viongozi wa Kanisa wanasikitishwa sana na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu huko Mashariki ya Kati zinazofumbiwa macho na viongozi wengi wa kimataifa kutokana na masilahi ya kisiasa na kiuchumi. Uhuru wa kweli, haki na amani, upendo, utu na heshima ya binadamu ni mambo ambayo ni msingi katika kukoleza maendeleo ya wengi. Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanaendelea kuhamasishwa na Kanisa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa Wakristo huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.