2015-03-31 14:57:00

Kiini cha Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma ya upendo


Alhamisi kuu tunaanza adhimisho lililo kuu kuliko maadhimisho yote ya Kilitutujia, adhimisho lililo chanzo cha maadhimisho yote ya kiliturujia. Hili ni adhimisho la FUMBO LA PASAKA, yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Liturujia yote ya Mama Kanisa mtakatifu inachota maana yake katika msingi huo. Adhimisho hili ni la siku tatu yaani: Ijumaa kuu tunayoianza siku ya Alhamisi kuu jioni kwa tukio la Karamu ya mwisho, Jumamosi kuu na Jumapili ya Pasaka.

Katika adhimisho la jioni ya Alhamisi kuu mambo matatu yanapewa uzito na tafakari ya kina katika kuelekea sherehe ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanza tunaadhimisha Karamu ya Bwana wetu Yesu Kristo, karamu hii huitwa Karamu ya mwisho ikiwa na maana ni Karamu ya mwisho ya Pasaka ambayo Kristo alikula pamoja na wanafunzi wake kabla ya kukamatwa kwake, kuteswa na kufa msalabani. Hivyo katika nafasi ya kwanza tunatafakari ukuu wa karamu hii ya kipasaka, karamu ambayo tofauti na Pasaka ya wayahudi, Kristo kama mkuu wa Kaya anaweka kitu kipya ambacho kinatupatia mwanzo mpya, mwanzo wa karamu ya mbinguni, karamu ambayo inatuunganisha na Baba, karamu ambayo inatufanya kuwa wana katika Mwana. Hii ni Ekaristi Takatifu, yaani, mwili na Damu ya Kristo katika maumbo ya mkate na divai.

Kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu kutuongoze katika tafakari yetu na kutoka kwake tuione maana ya Sakramenti ya Daraja Takatifu na Amri ya Mapendo. Maneno ya kuwekwa kwa Sakramenti hii tunayapata katika somo la pili ya siku hii ya leo: “Huu ndiyo mwili wangu” na “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu”. Vifungu hivi viwili vya Biblia vinaweka bayana kabisa maana ya Fumbo hili la Ekaristi Takatifu. Mkate ambao kwa kawaida ulitumika katika hafla hii ya kipasaka unapewa maana mpya, unakuwa si mkate tena wa kawaida bali ni Mwili wa Kristo. Mwanadamu anaunganishwa na Mungu tena kwa chakula hiki cha mbinguni. Divai ambayo ilikuwa ni kinywaji cha shukrani katika karamu ya kipasaka inakuwa si divai ya kawaida tena bali ni damu ya Kristo katika maumbo hayo ya divai.

Ekaristi Takatifu mlo wa kipasaka unabaki kuwa ni mlo wa kipasaka lakini unaunganishwa na Kristo mfufuka. Hivyo maumbo haya ya kawaida ya kibinadamu yanainuliwa katika hali ya juu kabisa na kupata hadhi ya juu. Hakika tunapaswa kujongea na kupokea katika hali ya uchaji mkuu, ni Yesu mfufuka, Yesu mzima ambaye amejitoa na amekufa kwa ajili yetu. Hakika mlo huu wa kipasaka ni Yesu mfufuka kwani Yeye mwenyewe alisema “huu ni Mwili wangu .... hii ni Damu yangu”. Hata baada ya ufufuko wake alidhihirisha muunganiko wa Kristo mfufuka na Kristo kabla ya ufufuko, aliwaonesha madonda yake mikononi na miguuni na pia pia ubavu uliotobolewa. Hapa walipata hakika ya Yeye aliyejitoa na kuteswa kwa ajili yetu na pia hapa mlo huu wa Kipasaka unapata maana kubwa na nzito, ukuwa chakula cha wokovu wetu.

Katika somo hilo la pili tunavumbua tena uwepo wa Maadhimisho  megine mawili ya siku ya Alhamisi kuu. Kristo katika kuuweka Mwili wake na Damu yake alimalizia kwa kutuma: “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Agizo hili la kuendeleza karamu hiyo ya kipasaka linatupeleka mara moja katika kutafakari ni kwa namna gani mlo huo utafanywa kuwa ni wa kudumu katika jamii ya mwanadamu. Fanyeni hivi ... ni agizo lakini pia linaendana na ruhusa ya kuendeleza tendo hilo. Kwa maneno mengine, mitume wanapokea uwezo wa kuendeleza tukio hilo, yaani, kugeuza mkate kuwa mwili wa Kristo na divai kuwa damu yake takatifu sana. Mwanadamu anapokea uwezo huo mkuu, uwezo wa kimungu, uwezo ambao unamfanya aweze hata kuamuru nguvu za uwinguni kushuka na kukaa nasi katika jamii yetu. Kwa agizo hili Pasaka hii ya kimbingu, Pasaka hii mpya ambayo inatuvusha kutoka katika utumwa wa dhambi na kutupeleka katika nchi ya ahadi ya Yerusalemu ya mbinguni inafanywa kuwa ni ya kudumu.

Hawa ndiyo Makuhani wetu ambao katika jumuiya yetu ya leo ya waamini wanamwakilisha Kristo, au kama tusomavyo katika lugha ya kilatini, lugha mama ya Kanisa, makuhani hawa huitwa “Alteri christi”, yaani, “Kristo mwingine”. Hivyo katika adhimisho hili la kipasaka tunaalikwa kwa namna ya pekee kuwaombea hawa watumishi wa matakatifu ya Mungu. Tuwaombee kwa dhati kwa namna ya pekee katika ulimwengu wetu huu wa leo, ulimwengu ambao umejaa kila aina ya upinzani, ulimwengu ambao yule mwana wa uovu, shetani, daima anazunguka tena kwa nguvu kubwa kuwateka hawa watumishi wa Mungu.

Ni dhahiri kwamba kila kuhani mkuu ametwaliwa kati ya wanadamu, lakini Neno la Mungu linaendelea kutuambia kwamba wamewekwa kati ya wanadamu kwa ajili ya mambo yamuhusuyo Mungu (Rejea Ebr 5:1). Hivyo, kuhani wetu, ingawa tunamwona ni mwanadamu mwenzetu bado anabakia kuwa si mwanadamu sawa tu na wanadamu wengine, anapaswa kutunzwa na kulindwa kwa sala na sadaka zetu ili shetani asimtwae na aendelee kusema “ndiyo” kwa milele katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu.

Uwepo huu wa daima wa Ekaristi Takatifu siyo wa mapambo, si jambo ambalo linakosa maana. Kristo anajiweka kwetu kama mlo ili tuushiriki mlo huo na kuneemeshwa kwa chakula hicho cha mbinguni. Ekaristi Takatifu inatupatia wajibu wa kuunganika na Kristo na kuwa ishara ya Upendo wake kwa watu wote. Tunakuwa kile tunachokipokea. Kama vile chakula cha kawaida kinavyokuwa cha faida kwa miili yetu kwa kutupatia nguvu na kukua kwa mwili, ndiyo chakula hiki cha kiroho kinakuwa nguvu na kutukuza katika maisha ya kiroho. Tunaunganika na Kristo na kufanywa kuwa yeye, yaani, tunayapokea maisha yake na kuyafanya kuwa ni maisha yetu. Yeye anakuwa ndiye chanzo cha utendaji wetu wa kikristo, kwa kumpokea tunafanywa kuwa vyombo vya kuisambaza habari njema ya Kristo kwa wanadamu wote.

Hili linatupeleka katika kutafakari jambo la tatu ambalo tunaliadhimisha siku ya Alhamisi kuu, yaani, Amri ya Mapendo.  Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa anatuambia maneno yafuatayo juu ya Ekaristi Takatifu, “Ni ishara ya Umoja na kifungo cha Upendo. Sakramenti ya Ekaristi ni Sakramenti ya Upendo”. Bwana wetu Yesu Kristo anatoa fundisho la namna ambayo upendo huo unapaswa kuwa; ni upendo wa kujitoa katika ukamilifu wote, kujisadaka katika uhuru wako mithili ya mtumwa. Namna yake ya utumwa ni tofauti na utumwa ulivyozoeleka. Anajitoa katika hali ya utumwa kwa uhuru wote na mapendo makubwa.

Anatambua wazi kwamba Yeye ni Bwana na mwalimu wao, ni mkuu wao na kwa desturi hakupaswa kuwaosha miguu walio chini yake. Hapa anatupatia shule kubwa sana ya namna ambavyo tunapaswa kujitoa kuwahudumia wengine katika hali ya Upendo mkamilifu. Siyo kuangalia nguvu zangu, mamlaka yangu, uwezo wangu n.k. bali ni kumwangalia mwanadamu mwenzangu aliye mbele yangu na anayehitaji huduma yangu, anayekuwa na hakika ya kupatiwa huduma hiyo kutoka kwangu.

Namna hii ya Upendo, inatuondoa katika kuhudumiana kwa ubaguzi wa namna yoyote na inatuleta katika umoja wa waana wa Mungu. Ishara hiyo ya umoja wa kikristo inakamilishwa na namna ambavyo Kristo anawaambia mitume wake alipo wagawia mkate waule na kikombe cha divai wanywe; Yeye mwenyewe anasema “Twaeni mle wote ... twaeni mnywe wote”. Kitu cha kushangaza ni kwamba pamoja na kujua kwamba yupo mmoja atakaemsaliti kati ya wanafunzi wake lakini bado haachi kuonesha Upendo huo mkuu. Ni upendo mkubwa wa kiasi gani? Hakika unatuunganisha bila kujali tofauti zetu katika chombo kimoja kama wanadamu. Ni mlo ambao unagawiwa kwa wote kuashiria Upendo wake wa kujitoa kwa wote bila kubagua. Na ndilo analotuagiza kulitekeleza akisema: “basi ikiwa mimi niliye Bwana na mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi”.

“Kama nisipokutawadha huna shirika nami”. Ni ujumbe kutoka Kristo anaopatiwa mtume Petro. Ujumbe huu unatupatia wazo moja la muhimu sana. Utume wetu na ushuhuda wetu wa kikristo si swala letu binafsi, si jambo la kujianzishia sisi wenyewe. Katika hatua ya kwanza tunapaswa kuoshwa na Kristo mwenyewe, yaani, kujiweka chini yake na kusikiliza na kuuelewa ujumbe wake. Mtume Petro alitambua wazi kwamba Kristo ni mkuu wao, alishakiri hapo nyuma kuwa ni mwana wa Mungu na hivyo aliona hastahili kutawadhwa miguu na Kristo.

Kristo anamfundisha kwa matendo maana ya utumishi anaoyotaka kuwaachia, namna ambavyo anataka wapendane. Hii inamaanisha kwamba tukitaka kujua namna ya kutenda kama Wakristo ni lazima kujiweka chini ya shule yake na kujifunza vile anavyofanya yeye. Mwanadamu katika udhaifu wake anaweka vikolombwezo vingi ambavyo mwishoni humfikisha katika usaliti na kuyachakachua mapenzi ya Mungu.

Hivyo, tunapoelekea sasa kutafakari mateso, kifo na ufufuko wa Bwana tuwe tayari kujiweka chini ya shule ya Krsito ili atutawadhe miguu, atakase nafsi zetu na kiburi cha kibinadamu, na upofu wa kibinadamu ili hatimaye tunapojongea kushiriki chakula cha kimbingu, Ekaristi Takatifu tuelewe na kuiona maana yake katika maisha yetu ya kila siku kama alivyotaka Bwana wetu Yesu Kristo na hivyo kuwa sawa na kile tunachokipokea.

TUMSIFU YESU KRISTO!

Na Padre Joseph Mosha.

Jimbo kuu la Dar es Salaam.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.