2015-03-31 15:31:00

Jubilee ya huruma ya Mungu, kumekucha!


Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuonesha nia ya kuadhimisha Mwaka wa huruma ya Mungu, hapo tarehe 13 Machi 2015 wakati alipokuwa anafanya kumbu kumbu ya miaka miwili tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, tarehe 11 Aprili 2015 atatoa Tamko rasmi kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilee ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anatarajiwa kuongoza Ibada ya Masifu ya Jioni kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia majira ya saa 11:30 kwa saa za Ulaya. Kabla ya maadhimisho ya Liturujia ya Masifu ya Jioni, Baba Mtakatifu atasoma baadhi ya vifungu muhimu kutoka kwenye Tamko la Jubilee ya Huruma ya Mungu, mbele ya Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Taarifa inaonesha kwamba, maadhimisho haya yanafanyika Jumapili ya Huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Kumbe, ni kipindi maalum kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani, tayari kupokea neema na rehema inayotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu, kumbu kumbu ya kufungwa rasmi kwa Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Tamko hili litabainisha mambo msingi yanayopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu yaani: ratiba, matukio muhimu yatakayoadhimishwa, nia ya maadhimisho haya na matunda yanayotarajiwa na Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Jubilee ya huruma ya Mungu kwa ajili ya Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, katika Jubilee maalum ambazo zimeadhimishwa na Mama Kanisa kwa miaka ya hivi karibuni ni ile ya Mwaka 1933 na Mwaka 1983; Matamko yake yalitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana au Epifani. Jubilee ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu inatangazwa rasmi wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu ili kukazia dhamana na changamoto iliyoko mbele ya Familia ya Mungu, ili kuweza kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya maisha ya Kisakramenti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.