2015-03-31 11:47:00

Endeleeni kusimama kidete kupinga vitendo vya kigaidi!


Maelfu ya wananchi waliokuwa wameandamana  na viongozi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, mwishoni mwa juma, walikusanyika mjini Tunis, Tunisia kupinga kwa nguvu zote vitendo vya kigaidi na kama alama ya mshikamano na wananchi waliopoteza maisha yao kutokana na shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye Jumba la Makumbusho ya kale la Bardo hivi karibuni. Jumuiya ya Kimataifa imependa kuonesha mshikamano na Serikali ya Tunisia katika kipindi hiki cha mpito kuelekea demokrasia ya kweli.

Hapa ni mahali ambapo cheche za mageuzi ya nchi za Kiarabu zilipoanzia na kuenea sehemu mbali mbali. Mara baada ya maandamano ya amani, Serikali ya Tunisia, imezindua bango la majina ya watu  22 waliofariki dunia kutokana na shambulizi la kigaidi lililofanyika tarehe 18 Machi 2015. Wananchi wengi wa Tunisia wameshiriki kwa hali na mali katika maandamano haya kupinga vitendo vya kigaidi vinavyofanywa dhidi ya watu wasiokuwa na hatia.

Ni matumaini ya wananchi kwamba, Serikali pamoja na wadau mbali mbali wataendelea kushikamana kwa dhati kupinga vitendo vya kigaidi, ili kudumisha misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu.

Na mwandishi wetu!

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.