2015-03-30 11:33:00

Wakristo wanahamasishwa kutetea na kutunza mazingira!


Wakristo nchini Cambodia wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kulinda na kutunza mazingira kwa kushinda kishawishi cha kuchafua mazingira. Wanahamasishwa kufanya funga ya kiekolojia, kwa kuheshimu mazingira ambayo ni masikani ya viumbe hai.

Lengo la tafakari hii kutoka kwa Wayesuit wanaofanya utume wao nchini Cambodia ni kuwasaidia waamini kutunza vyema afya zao kwa kuzingatia kanuni maadili, kwani waathirika wakubwa wa uchafuzi wa mazingira ni wananchi wa kawaida na maskini ambao hata pengine hawana fedha ya kugharimia chakula, dawa pamoja na mahitaji yao msingi.

Waamini wanahamasishwa kubadili mfumo wa maisha yao pamoja na kushiriki katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira ambayo kwa sasa yanaharibiwa sana kutokana na wafanyabiashara wanaotafuta faida kubwa kwa gharama ya  maisha ya wananchi wa Cambodia. Kutokana na uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji, wananchi wengi wanajikuta wakishambuliwa na magonjwa ya milipuko; mambo ambayo yamekuwa ni chanzo kikubwa cha maafa ya wengi.

Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuna maeneo ambayo yanakabiliwa na ukame wa kutisha ambao umepelekea uwepo mkubwa wa uhaba wa chakula na matokeo yake watoto wengi wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo wa kutisha. Kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa Kifua kikuu, Malaria na Ukimwi.

Kwaresima kiwe ni kipindi kinachowawezesha waamini kuingia katika Jangwa la maisha yao ya ndani, ili kutafakari kuhusu changamoto za maisha na kuangalia jinsi wanavyowajibika kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora kama sehemu ya mchakato wa maboresho katika afya zao. Waamini wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi na pale inapobidi kuacha kutumia magari, ili kupunguza uchafuzi wa mazingira unaofanywa kwa kuzalisha hewa ya ukaa kutokana na mashi wa magari.

Waamini washiriki katika upandaji na utunzaji wa miti. Huu ni mchakato unaopania waamini kujipatanisha na mazingira, kupembua tena mambo msingi katika maisha na kuwa na matumizi bora zaidi ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya mafao ya wengi. Huu ni mchakato wa haki ya mazingira, unaosimamiwa na makundi makubwa ya Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.