2015-03-30 14:15:00

Njia ya Msalaba Ijumaa kuu: Wakristo wanahamasishwa kulinda!


Baba Mtakatifu Francisko amemkabidhi Askofu mstaafu Renato Corti wa Jimbo Katoliki Novara, Italia kuandaa tafakari ya Njia ya Msalaba itakayotumika wakati wa Njia ya Msalaba, Ijumaa kuu tarehe 3 Aprili 2015 kuzunguka Magofu ya Colosseo. Itakumbukwa kwamba, kunako mwezi Februari 2005 aliongoza mafungo kwa Mtakatifu Yohane Paulo II na wasaidizi wake wa karibu.

Upendo unaolinda ndilo wazo kuu litakayoongoza tafakari za Vituo vya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Colosseo yaliyoko mjini Roma, uwanja uliokuwa unatumiwa na Warumi kwa ajili ya kuwashindanisha binadamu na wanyama wakali! Ni maneno ambayo yalitamkwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mtakatifu Yosefu alipewa dhamana ya kumlinda Bikira Maria na Mtoto Yesu. Hata leo hii waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni vyombo vya kutunza na kudumisha upendo kwa binadamu.

Kulinda ni neno ambalo limetumiwa sana na Mtakatifu Paulo katika nyaraka zake kuhusu upendo wa Mungu na maelekeo yake. Askofu Corti anasema, neno hili kulinda linagusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: Ni neno ambalo linajikita katika Maandiko Matakatifu, Fumbo la Ekaristi na Huruma. Tafakari hii inajikita katika tunu msingi za maisha ya familia kwa kuingiza pia sala ya kuombea Sinodi, ili kweli huruma na ukweli viweze kuwasindikiza waamini katika hija ya maisha yao ya kiroho. Ni tafakari inayolenga kupyaisha maisha na utume wa Kanisa pamoja na mapungufu yanayojitokeza katika ulimwengu mamboleo, lengo msingi likiwa ni kulinda.

Askofu mstaafu Corti anasema, kuna dhambi zinazofanywa dhidi ya vijana wa kizazi kipya; maskini kutelekezwa; jamii kupuuza misingi ya haki na amani kama ilivyobainishwa na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume, Amani Duniani, Pacem in Terris, yaani: ukweli, haki, uhuru na upendo. Ni tafakari inayogusa kwa undani zaidi changamoto katika ulimwengu mamboleo kwa mfano: adhabu ya kifo inayopaswa kufutwa duniani; tabia ya watu kukumbatia utamaduni wa kifo kwa vitendo vya utoaji mimba na mauaji ya kikatili kama yanavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia bila kusahau biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Askofu mstaafu Corti anasema hata leo hii bado kuna watu wanaoendelea kujisadaka ili kuwatangazia walimwengu Injili ya Matumaini. Hawa ni Wamissionari waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia kama umande wa asubuhi, wanavoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia na kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi na hatimaye, kuwakirimia utu na heshima yao kama watoto wapendwa wa Mungu.

Askofu mstaafu Corti anasema, ni jambo lisilokubalika kwa baadhi ya watu ndani ya jamii kutumia dini ili kufanya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na kwa jili ya mafao yao binafsi. Mauaji, kinzani na migogoro inayoendelea kujitokeza ni changamoto kwa waamini kujikita katika Injili ambayo kweli ni mlinzi mkuu wa binadamu, utu, heshima na ustawi wake. Yaani watu wanapata bahati kubwa ya kuweza kukutana na Yesu kwa njia ya Neno lake. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa na hali ya giza lakini pia kuna mwanga unaojionesha hata kama umefifia kiasi gani!

Hapa Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaalikwa kuanza upya, kuwa na ujasiri, tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni wakati wa waamini Barani Ulaya kujifunza kutoka Afrika, mahali ambapo watu wanatembea umbali mrefu ili kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu, lakini waamini ambao Makanisa yako mbele ya nyumba zao, wameshikwa na uvivu kiasi kwamba, hawaoni tena sababu ya kwenda Kanisani.

Tafakari ya Njia ya Msalaba iliyoandaliwa na Askofu mstaafu Renato Corti inavionjo vya maisha ya kiroho, kwani simulizi yake inamshirikisha mwamini kuandamana na Yesu, kwa kumpatia maneno ya kusema. Yesu anazungumza na mtu binafsi kutoka katika undani wake na wakati mwingine anajibiwa na umati mkubwa wa watu wanaokutana naye katika Njia ya Msalaba. Haya ni majadiliano yanayowashirikisha waamini katika Njia ya Msalaba, kwa kumwangalia Yesu na wale wote wanaomzunguka.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.