2015-03-30 10:44:00

Maadhimisho ya Juma kuu


Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi chetu cha Hazina Yetu, Tumsifu Yesu Kristo! Katika kipindi hiki ninakualika tuzungumze kidogo juu ya Juma Kuu. Juma Kuu ni wiki ambayo sisi Tunaomsadiki Kristo, tunaadhimisha matukio ya imani yanayorandana na siku za mwisho za Kristo, hasa yakijumuishwa mafumbo ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo.

Juma kuu huanza Dominika ya Matawi hadi Jumamosi kuu, yaani siku inayotangulia Pasaka, siku ambayo tunakumbuka Kristo alipofufuka kutoka kwa wafu. Pasaka kwetu sisi Wakristo, ni Sherehe kubwa, tunayoisherehekea kila mwaka katika Dominika ya Mwezi Mpevu ambayo huwa kati ya mwezi Machi na Aprili ya kila mwaka.  Adhimisho hili, ndio utimilifu wa maisha, mafundisho, miujiza, na matendo yote ya Kristo katika kumkomboa mwanadamu. Sasa tuone kila adhimisho katika upekee wake.

Jumapili ya Matawi

Juma kuu ambalo huanza na adhimisho la Dominika ya Matawi, Katika Dominika hii sisi tunaomsadiki Kristo, tunakumbuka na kudhimisha siku ile Bwana alipoingia Yerusalemu kwa shangwe. Siku ile ambapo, Makutano walimkiri na Kumwimbia kuwa ni ‘Masiha, Mwana wa Daudi’. Na kwa imani waliokuwa nayo kwa huyo Masihaq walikuwa wakimwomba awasaidie wakisema ‘Hossana’, maana yake Okoa SASA!

Na sisi katika kuadhimisha Dominika ya Matawi, tunakumbuka pia hali ya nyakati zetu, nyakati tete ambapo dunia yetu imekuwa si mahali salapa tena. Matumaini ya maisha ya uhuru na amani yanapotea. Vikao vingi vya viongozi wa dunia havizai matunda sana. Mwanadamu amegubikwa na mahangaiko, hofu, wasiwasi na kukata tamaa ya maisha. Damu za wanadamu zinaimwagilia ardhi kila siku. Familia ya mwanadamu imeshetanishwa na shetani anatawala kwa nguvu na kasi ya ajabu. Tufanyeje sisi? Tuendelee kusali bila kuchoka, tuimbe kwa Yesu tukisema ‘ Hosana’, utuokoe Sasa.

Baada ya Dominika ya matawi tuna siku ya Jumatatu, Jumanne na Jumatano ya Juma kuu. Katika siku hizi tunakumbuka zaidi kusalitiwa kwa Kristo. Yuda alimsaliti Kristo kwa fedha. Somo la Kwanza katika siku hizi linamwelezea Kristo kama Mtumishi Mteswa, kama tusomavyo kutoka katika kitabu cha Isaya.

Katika Siku hizi, tukumbuke juu ya usaliti uliojaa katika maisha yetu. Kristo alipoulizwa juu ya dalili za mambo ya mwisho alipokuwa katika mlima wa  Mizeituni, moja ya ishara, alisema ‘ watu wataacha imani yao na kusalitiana’. Lakini usaliti huu haupo katika imani tu, upo katika mahusiano na matendo ya kila siku ya maisha yetu. Na yawezekana, kuna siku uliwahi kujisaliti mwenyewe kabisa ukajiweka katika matata makubwa. Tunapotafakari usaliti wa Yuda, tunataka sisi kujenga zaidi uaminifu wetu kwa Mungu ambaye tulimwahidia kwa viapo katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara kwamba tutalinda vema imani yetu. Na pia tunataka kuomba neema ya kujijenga na kuishi katika dhamiri njema, ili tukwepe kabisa kila aina ya usaliti, uwe wa hadharani au wa sirisiri.

Baada ya Siku hizo tatu, litafuata adhimisho la Misa ya Krisma, ambamo Makuhani wote katika Jimbo, pamoja na waamini hukutanika katika misa inayoadhimishwa katika Kadhedrali. Katika misa hiyo, Mapadre hurudia viapo vya upadre wao wakiongozwa na Askofu wao. Katika misa hii, yanabarikiwa mafuta ya Wakatekumeni na ya Wagonjwa, kisha yanawekwa Wakfu mafuta ya Krisma ambayo hutumika kwa maadhimisho ya Sakramenti za: Ubatizo, Kipaimara na Daraja takatifu

Siku hii, tuwaombee sana Mapadre wetu, amani, uimara na usitawi, na hasa mapadre wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira magumu ya vita, manyanyaso ya kidini na mauaji. Wanateseka kwa wasiwasi, na wanaumia kondoo wao wanavyochinjwa kama wanyama tu. Mungu awasaidie, na sala zetu ziendelee kuwategemeza.

Baada ya Adhimisho hilo la Misa ya Krisma, yanafuata sasa Maadhimisho ya Siku Tatu Kuu za Pasaka.  Tunaanza na Alhamisi Kuu Jioni, ambapo tunaadhimisha sadaka ya Misa Takatifu Jioni, tukikumbuka Karamu ya Mwisho. Katika karamu hii tunakumbuka pia kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Daraja Takatifu. Katika Adhimisho la Karamu ya Mwisho, Kristo Bwana alifanya tendo la kuwaosha wanafunzi wake miguu, alama na mwaliko wa utumishi mwema na mnyenyekevu kwa wote. Tuwe tayari kuwahudumia kwa huruma na upendo binadamu wenzetu, huku tukitupia jicho laini kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kisha linafuata adhimisho la Ijumaa kuu, ambapo ulimwengu wote unagubikwa giza la huzuni ukikumbuka  mateso na kifo cha Bwana, pale juu msalabani. Ibada hii, popote duniani huanza saa tisa  za alasiri. Pamoja na sehemu ya Liturijia ya neno, na mwisho Liturijia ya Ekaristi Takatifu, tunalo tendo la kuabudu Msalaba Mtakatifu wa Bwana, ambao haswa ni altare ya Kwanza ambapo Kristo Mwenyewe aliadhimishia sadaka ya Mateso na Kifo chake. Ni Kristo akiwa pale msalabani na achomwa ubavu wake kwa mkuki, hapo ikatoka damu na maji; ndipo zilipozaliwa Sakramenti za Kanisa. Hivyo kuabudu kwetu Msalaba kunafumbata uzito wa matukio na mafundisho.

Tena katika hili, tusipindishe maneno, Sisi Wakristo tena hasa Wakatoliki, tunauabudu Msalaba Mtakatifu wa Bwana. Kwetu sisi ni chombo cha Ukombozi ndiyo maana tunasali tukisema, Ee Yesu Tunakuabudu na tunakuheshimu, wewe uliyetukomboa kwa Msalaba wako Mtakatifu. Mkristo, Usilikose tendo hili la Ibada na adimu. Siku hiyo ya Ijumaa kuu, usihasau mpendwa Msikilizaji, tunaambiwa, Usile nyama Siku ya Ijumaa kuu. Zaidi ya yote, ni siku ya Mfungo Mkuu.

Jumamosi Kuu

Siku hii, kama ilivyo Ijumaa kuu, hatuadhimishi Misa Takatifu. Sakramenti ya Wagonjwa hupelekwa tu kwa wale walio katika hatari ya kufa. Usiku, tunaadhimisha Mkesha Mtakatifu wa Pasaka, au Vijilia ya Pasaka. Maadhimisho ya usiku huu Mtakatifu kwa sisi Wakatoliki, ndiyo yanabeba umuhimu wa juu kabisa ukilinganisha na maadhimisho mengine yote. N ikiini na chemchemi ya Ibada nyingine zote. Katika haya kuna Ibada ya kubariki moto, na kisha Ibada ya Mwanga. Liturujia ya Neno ina masomo 7 ya agano la Kale na 2 ya Agano Jipya. Kisha liturujia ya neno, inafuata Liturujia ya Ubatizo, ambapo waamini wote tunarudia ahadi zetu za Ubatizo. Kisha Misa inaendelea kama Kawaida na tayari kwa maadhimisho haya tunakuwa tumekwisha kuingia katika maadhimisho ya Sherehe za Pasaka.

Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi chetu cha Hazina Yetu, tunakutakia maadhimisho mema ya Juma Kuu na Baraka za Kristo Bwana ziwe nasi Daima.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.