2015-03-29 10:27:00

Njia ya unyenyekevu ni mtindo wa maisha ya Mungu na Wakristo!


Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili ya matawi, sanjari na maadhimisho ya Siku ya 30 ya Vijana Kimataifa, ambayo kwa mwaka 2015 inaadhimishwa katika ngazi ya kijimbo, wameshiriki maandamano makubwa ya matawi, kuzunguka Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maadhimisho haya ni kumbu kumbu endelevu ya siku ile Yesu alipoingia kwa shangwe mjini Yerusalemu na watu wakatandika nguo zao njiani na kumshangilia kwa sauti za shangwe kiasi cha kuwashangaza wengi. Kwa mwaka huu, wawakilishi 200 wa vijana kutoka nchi mbali mbali wameshiriki kuipamba siku ya vijana kimataifa ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu ”Heri wenye moyo safi”.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekumbusha kwamba, licha ya siku hii kuonekana kuwa ni ya shangwe kuu, lakini inaongozwa na fadhila kuu ya “unyenyekevu” inayowafunuliwa watu mtindo wa maisha ya Mungu na kwa Wakristo, fadhila ambayo itaendelea kuwashangaza wengi, kwani watu hawajazoea kumwona Mwenyezi Mungu anayejinyenyekesha kiasi cha hata kudiriki kufanya hija na watu wake, akiwavumilia hatapale walipokosa uaminifu kwake.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mwenyezi Mungu aliendelea kuwa msikivu hata pale watu wake walipomnung’unikia, wakamlalamikia na kumpinga wazi wazi. Ni watu waliokuwa na shingo ngumu waliosahau kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Baba yao aliyewakomboa kutoka utumwani, akawavusha salama jangwani, ili kuwapeleka kwenye Nchi ya ahadi na uhuru.

Maadhimisho ya Juma Kuu yanawaingiza Wakristo katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, changamoto kwa waamini kufuata njia ya unyenyekevu ulioneshwa na Yesu, ili kuweza kushiriki kikamilifu utakatifu wa Juma kuu. Ni kipindi cha kusikiliza mashitaka yaliyoletwa na wakuu wa Makuhani ili kumwangamiza Yesu; ni kipindi cha kumwona Yesu anakamatwa, anateswa na kukimbiwa na Wafuasi wake kana kwamba ni mnyang’anyi wa kutupwa.

Yesu atapelekwa mbele ya Baraza kuu la Wayahudi, watamkejeli na hatimaye atahukumiwa kifo. Petro aliyetajwa kuwa ni mwamba, atamkana Yesu mara tatu; watu watapiga kelele wakitaka Baraba aachiliwe huru na Yesu asulubiwe! Atavikwa vazi la rangi ya zambarau na kutiwa taji la miiba kichwani, tayari kuanza Njia la Msalaba, atachekwa na wakuu wa Makuhani kwa kujifanya kuwa Mfalme na Mwana wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo njia Mungu, njia ya unyenyekevu inayojikita katika huduma, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine kama yanavyosema Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Njia ya Msalaba ni tofauti kabisa na njia inayomezwa na malimwengu kwa kuwatumbukiza watu katika maisha ya fahari, kiburi na mafanikio; mitego ambayo Shetani anaitumia, kama alivyofanya kwa Yesu kule jangwani kwa muda wa siku arobaini, lakini Yesu akaibuka kidedea. Waamini wanaweza kupata pia ushindi si kwa kujikita katika matukio makubwa tu ya maisha, bali katika kila hatua ya maisha yao ya kila siku. Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha fadhila ya unyenyekevu  kwa ajili ya huduma kwa jirani, wagonjwa, wazee na wasiojiweza.

Unyenyekevu huu unaoneshwa pia na waamini wanaoendelea kuwa waaminifu kwa Injili ya Kristo; wanatengwa na kunyanyaswa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, hawa anasema Baba Mtakatifu ndio mashuhuda wa imani kwa nyakati hizi. Ni kundi ambalo linashuhudia kwa njia ya maisha na ujasiri ile Njia ya Msalaba. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufuata njia hii kwa ukamilifu zaidi, kwa kuonesha upendo kwa Yesu Kristo Bwana na Mwokozi na kwamba, ni upendo utakaowaongoza na kuwapatia nguvu, ili kuandamana pamoja na Yesu Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.