2015-03-28 09:41:00

Mahusiano kati ya Askofu na Watawa katika Makanisa mahalia!


Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, imebainika kwamba, kuna haja ya kujenga, kuimarisha na kudumisha mahusiano kati ya Maaskofu na Watawa wanaotekeleza dhamana na majukumu yao katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, kama ambavyo waliwahi kusema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican hatika Waraka wa Mapendo Kamili, Perfectae caritatis. Maaskofu na watawa hawana budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake, kama kiungo muhimu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Angelo Massafra, Makamu wa Rais, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE, wakati alipokuwa anatoa hotuba kwa viongozi wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume yanayofanya utume wao Barani Ulaya. Mkutano huu umefanyika mjini Tirana.

Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wao si muhtasari wa karama za Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, bali wao ni kielelezo cha umoja wa karama; jambo linalooneshwa na huduma ya kichungaji inayopaswa kutolewa na Maaskofu ili kuwasaidia watawa kutekeleza utume na maisha yao barabara katika Makanisa mahalia. Maaskofu na watawa wajenge moyo wa udugu na urafiki unaojikita katika mahusiano bora kati ya Baba na mwana.

Maaskofu wajenge na kudumisha utamaduni wa majadiliano, ili watawa waweze kuchangia katika ustawi na maendeleo ya Makanisa mahalia badala ya Maaskofu kuwa ni vikwazo, hali ambayo inawakatisha watawa kuchangia kikamilifu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia, kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za dunia. Watawa wasaidiwe na Maaskofu kutumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Ili kufanikisha azma hii, Maaskofu wajibidishe kutambua, kuthamini na kupokea karama hizi kwa ajili ya ustawi wa Kanisa mahalia, kwani huu ni wito na karama ya Mashirika husika. Askofu asiwe ni kikwazo cha zawadi ya Roho Mtakatifu kwa Makanisa mahalia, bali asaidie kutambua karama hizi kwa mwanga wa mang’amuzi ya kibaba, tayari kuwasaidia watawa, mashirika ya kitawa na vyama vya kitume kuwashirikisha wengine.

Watawa wamekumbushwa kwamba, wito na maisha yao si mbadala wa utume na maisha ya Kanisa, bali watambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, wanaotekeleza utume wao wa kinabii, daima wakijitahidi kumfuasa Yesu Kristo Mwalimu na mchungaji mwema. Maaskofu na watawa wakijenga utamaduni wa kumsikiliza Roho Mtakatifu kwa hakika wataweza kushirikiana kwa dhati na watawa wa mashirika mbali mbali.

Roho Mtakatifu awasaidie watawa kuwaamsha walimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mashiko na mvuto katika maisha na huduma wanayotoa kwa Familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Watawa wawe ni wajenzi wa madaraja ya udugu, upendo na mshikamano wa dhati; wakionesha kwamba, inawezekana kuishi kwa upendo hata katika tofauti msingi na kwamba, upendo wa dhati ni jambo linaloweza kumwilishwa katika maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.