2015-03-28 15:32:00

Kijana usichezee kazi, chezea mshahara ni haki na mali yako!


Padre Tumaini Litereku kutoka Jimbo kuu la Songea, Tanzania wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya 30 ya Vijana katika ngazi ya Kijimbo anatafakari kwa ufupi, Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake, akiwataka vijana kuzifahamu, kuzitafakari na hatimaye kuzimwilisha katika uhalisia wa maisha yao, ili waweze kuheshimiwa hapa duniani na hatimaye kupata maisha ya uzima wa milele!

Padre Litereku mwanafunzi mtaalam wa Maandiko Matakatifu anabainisha kwamba, Heri nane zinawachangamotisha vijana kuridhika katika maisha yao, kuwa watu wa haki na vyom bo vya amani; kufanya kazi kwa juhudi na maarifa pamoja na kuhakikisha kwamba, wanajiepusha na tamaa pamoja na kutafuta njia za mkato ili kufanikisha maisha yao.

Vijana watambue kwamba, mambo mazuri hayataki haraka na kupanga ni kuchagua. Vijana wajifunze kuwa na subira, maadili, imani na utu wema. Vijana wasipokuwa thabiti watamezwa na malimwengu na matokeo yake: watakuwa ni wala rushwa na mafisadi wakubwa; wabwia unga na wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya;  wasipokuwa makini watajikuta wanapiga kwata ya ukahaba kwenye mitaa mjini na vijijini.

Vijana wanapaswa kuwa na juhudi na maarifa katika kazi, masomo na maisha katika ujumla wake. Kwa wafanyakazi wasithubutu kuchezea kazi kwani ni mali ya mwajiri, wakitaka wanaweza kuchezea mshahara kwani ni haki na mali yao. Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu. Kipato kiwe ni matunda ya bidii, juhudi na maarifa na kamwe wasitafute njia ya mkato!

Vijana wanapaswa kupambana umaskini wa hali na kipato hadi kieleweke. Yesu katika mafundisho yake anakazia umuhimu wa umaskini wa roho na usafi wa moyo kama nyenzo ya kupata maisha ya uzima wa milele. Vijana wajifunze kujikatalia anasa na kamwe wasikubali kuwa ni bandari ya tamaa, kwani wanaweza kumezwa na majanga katika maisha na huko watakiona cha mtema kuni! Vijana wasikubali kukimbizwa mchaka mchaka kwa kukubali mashinikizo ya ujana, kwani fainali ziko uzeeni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.