2015-03-27 11:44:00

Tarehe 29 Machi 2015, Siku ya Sala kwa Wakristo Mashariki ya Kati!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linawaalika Wakristo wa Makanisa yote, kusali na kuwaombea Wakristo huko Mashariki ya Kati, Jumapili tarehe 29 Machi 2015, Kanisa linapoadhimisha Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu, linalowaingiza waamini kutafakari: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka katika wafu. Huu ni mwaliko ambao umetolewa na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa kidugu.

Vita, dhuluma na nyanyaso zinatishia uwepo endelevu na mchango ambao umetolewa na Wakristo huko Mashariki ya kati katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu kwa kuzingatia tofauti zao za kiimani mambo msingi yanayosaidia kuimarisha mfungamano wa kijamii kati ya watu. Baraza la Makanisa anasema Dr. Tveit katika kipindi hiki cha Kwaresima,  limewasindikiza Wakristo huko Mashariki ya Kati kwa njia ya sala na sadaka, hasa wakati huu wanapojisikia kwamba, hawana nguvu tena ya kuleta mabadiliko katika hatima ya maisha yao.

Katika kishawishi cha kukata na kujikatia tamaa, hapa kuna haja ya kuonesha moyo wa upendo na mshikamano, ili kuwaimarisha na kuwatia nguvu Wakristo huko Mashariki ya Kati, ili waweze kusonga mbele licha ya magumu wanayokabiliana nayo kwa wakati huu. Wakristo wanapaswa kuyasimika maisha na matumaini yao kwa Mwenyezi Mungu kwani baada ya Ijumaa kuu, kuna chereko chereko na nderemo za Kristo Mfufuka.

Imani na matumaini ni chanda na pete katika maisha na ushuhuda wa Wakristo mbele ya mateso na mahangaiko ya mwanadamu. Bila utani, Wakristo wanateseka sana huko Iraq, Syria, Libia, Misri na Nigeria. Wanashambuliwa na silaha kali na waamini wenye misimamo mikali ya kiimani. Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha idadi kubwa ya Wakristo waliokwisha kuuwawa huko Mashariki ya Kati kutokana na chuki za kiimani. Wakristo wanauwawa na kunyanyaswa kiasi cha kukimbia makazi yao, ili kuokoa maisha. Ndiyo maana Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya sala ili kumlilia kwa ajili ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, anasema Dr. Olav Tveit.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.