2015-03-27 12:14:00

Kanisa nchini Syria linaomboleza kifo cha Patriaki Mar Dinkha wa IV


Patriaki Mar Dinkha wa IV wa Kanisa la Syria amefariki dunia Alhamisi tarehe 26 Machi 2015 huko Rochester, Minnesota, Marekani aliokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa mapafu. Marehemu Patriaki Dinkha wa IV alizaliwa kunako tarehe 15 Septemba 1935. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 15 Julai 1957. Tarehe 11 Februari 1962 akawekwa wakfu kuwa Askofu na kuwa Patriaki kunako mwaka 1976 baada ya Patriaki Eshai Shimun kuuwawa kikatili. Katika maisha na utume wake, alibahatika kukutana na kuzungumza na Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko.

Ni kiongozi aliyejisadaka maisha yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini Syria, akahakikisha kwamba, watu wanajikita katika misingi ya haki, amani, ukweli, umoja na upatanisho wa kitaifa. Alihimiza majadiliano ya kiekumene na kidini, ili kuimarisha maridhiano kati ya watu. Marehemu Patriaki Mar Dinkha wa IV anatarajiwa kuzikwa tarehe 8 Aprili 2015, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu George mjini Chicago, Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.