2015-03-27 09:26:00

Kanisa mbele ya Fumbo la Wokovu


Baba Mtakatifu Francisko, viongozi wakuu wa Vatican na wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume, Ijumaa tarehe 27 Machi 2015 wameshiriki katika mahubiri ya nne na ya mwisho kwa kipindi cha Kwaresima, ambayo yamekuwa yakitolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka.

Imani inayoyaaunganisha Makanisa ya Mashariki na Magharibi kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza tafakari za Padre Cantalamessa katika kipindi hiki cha Kwaresima. Maisha ya Kikristo kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki ni kuwasaidia kufanana na Mungu na kwamba, Fumbo la Umwilisho linawasaidia kurejesha tena ile sura na mfano wa Mungu. Kwa Makanisa ya Magharibi maisha ya Kikristo ni kutafuta utakatifu na Fumbo la Umwilisho ni kwa ajili ya kulipa fidia na kutenda haki.

Padre Cantalamessa anabainisha kwamba, kuna mambo makuu mawili katika wokovu kadiri ya Maandiko Matakatifu; Agano la Kale na Agano Jipya na la milele. Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu na kumwaga damu yake ili iwe ni fidia kwa wengi. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, watu wamehesabiwa kuwa  haki na kukirimiwa: neema na amani katika Mungu na kwamba: imani na matumaini ya upendo wa Mungu yamekwisha kumiminwa mioyoni mwa waamini kwa njia ya Roho Mtakatifu waliompokea.

Hapa Mama Kanisa anawataka watoto wake kuwa na mwelekeo chanya kwamba, kwa njia ya Fumbo la Pasaka wamekirimiwa tena ile sura na mfano wa Mungu pamoja na kukombolewa katika dhambi. Dhambi ni ukuta uliomtenganisha mwanadamu na Mwenyezi Mungu, ukabomolewa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.  Sakramenti ya Ubatizo inamwondolea mwamini dhambi ya asili na kuwa ni kiumbe kipya katika Kristo.

Roho Mtakatifu anawaimarisha waamini kuishi katika neema ya Mungu kwa kuondokana na dhambi za mauti. Neno la Mungu linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha ya waamini sanjari na kujitahidi kuunganisha taalimungu na tasaufi, ili kuweza kufahamu vyema maana ya wokovu katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Huu ni wito unaoendelezwa na vyama vya kitume kama fursa na nafasi ya pekee kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, kama alivyobainisha Mwenyeheri Paulo VI alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Upyaisho wa Roho Mtakatifu.

Mtakatifu Yohane XXIII anatambua kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni chachu kubwa ya mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki, kwa kutambua karama za Roho Mtakatifu zinazofanya kazi ndani ya Kanisa na leo hii kuna vyama vingi vya kitume, matunda na kazi ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya vyma hivi waamini wengi wameweza kukumbatia tena imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; wameonja umuhimu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika imani tendaji; chachu kubwa ya mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa.

Roho Mtakatifu hawezi kamwe kubinafsishwa na baadhi ya waamini ndani ya Kanisa na waamini nao waguswe na kutikishwa na neema hii inayotenda kazi ndani ya Kanisa. Karama mbali mbali hazina budi kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, kwa kukita maisha kwa Kristo na Roho Mtakatifu.

Ni matumaini ya Padre Raniero Cantalamessa kwamba, maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kitume cha Upyaisho wa Kikatoliki, yatakayofanyika kunako mwaka 2017 kwa kuwakutanisha Mapadre kutoka sehemu mbali mbali za dunia, itakuwa ni fursa ya umwilishaji wa karama a Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Padre Raniero Cantalamessa anahitimisha tafakari za Kipindi cha Kwaresima, kwa kuwataka wasikilizaji wake kumfungulia Roho Mtakatifu malango ya mioyo na maisha yao ili kuona jinsi Makanisa ya Mashariki na Magharibi yanavyounganishwa katika imani moja, ushuhuda na mshikamano wa udugu na upendo kati ya Makanisa. Amewatakia maandalizi na hatimaye, maadhimisho mema ya Siku kuu ya Pasaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.