2015-03-26 09:36:00

Utamaduni wa maisha ni urithi wa binadamu!


Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inajenga na kudumisha utamaduni wa maisha kwani huu ni urithi wa binadamu wote. Ni mwaliko wa kusoma na kutafakari kwa mara nyingine tena, urithi mkubwa ulioachwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Injili ya Uhai, miaka ishirini iliyopita. Huu ni ujumbe endelevu kwani Mama Kanisa anatambua na kuthamini utu na heshima ya kila binadamu kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni mambo yanayotishia kwa kiasi kikubwa Injili ya Uhai kwa kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo. Monsinyo Jean Marie Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la huduma ya kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anawahamasisha Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai.

Hii ndiyo maana, Kanisa sehemu mbali mbali za dunia, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, yaani tarehe 25 Machi, limeadhimisha Siku ya Injili ya Uhai duniani kwa sala na tafakari kwa maandamano na ushuhuda wa Injili ya Uhai. Bikira Maria kupashwa habari ya kuwa ni Mama wa Mkombozi ni mwanzo wa maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho, ndiyo maana Mama Kanisa yuko mstari wa mbele kutetea Injili ya Uhai kwani hii ni sehemu ya utume na dhamana yake ya kichungaji.

Monsinyo Mupenda watu ameyasema haya wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume, Injili ya Uhai kama sehemu ya mwendelezo wa mafundisho ya kina kuhusu maisha ya mwanadamu yaliyotolewa na Mwenyeheri Paulo VI, Humanae vitae pamoja na Waraka wa Wajibu wa Familia za Kikristo, Familiaris consortio. Waamini wanahamasisha kusimama kidete kutangaza Injili ya Uhai, Injili ya Familia na kukataa katu katu kumezwa na utamaduni wa kifo.

Waamini na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa kukumbatia kweli za Kiinjili na Kanuni maadili kama zilivyobainishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II “Mng’ao wa ukweli” Veritatis splendor”. Nyaraka zote hizi za Mama Kanisa zinalenga kutetea na kuendeleza Injili ya Uhai kwa kuheshimu na kuthamini uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mkesha wa Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mkombozi, imeadhimishwa kwa njia ya tafakari, sala na Ibada ya Misa Takatifu, ili kuombea zawadi ya maisha, watu waweze kuwa na ujasiri wa kulinda, kutetea na kuendeleza maisha ya mwanadamu tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya familia amewataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa mashuhuda wa Injili ya Uhai, kwa kuwasaidia na kuwahudumia wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi pamoja na kuwasaidia mashuhuda wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza Injili ya Uhai na Familia.

Waamini waendelee kujielimisha kuhusu umuhimu wa Injili ya Uhai, kwa njia ya: sala, katekesi makini lakini hasa kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya imani inayomwilishwa katika matendo, kwa kukubali na kupokea zawadi ya maisha. Mama Kanisa hataki kumhukumu mtu, anapenda kumwonjesha mwanadamu huruma na upendo wa Mungu na kumjengea matumaini, ili kuendelea kuthamini na kutunza ile sura na mfano wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya Injili ya Uhai na Injili ya Familia kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 25 Machi 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.