2015-03-26 09:48:00

Ndoa takatifu ni kati ya Bwana na Bibi! Mengine ni majanga tu!


Askofu mkuu Salvatore Cordileone wa Jimbo kuu la San Francisko, Marekani katika barua yake ya wazi kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Marekani anabainisha kwamba, Mama Kanisa anapenda kusimama kidete: kufundisha, kulinda na kudumisha Injili ya Familia inayojikita katika mapendo ya dhati kati ya bwana na bibi kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Wanandoa wanakuwa na wajibu na dhamana ya kulinda na kudumisha Injili ya Uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Kutokana na dhamana hii, Kanisa pia linapenda kuwalinda na kuwahudumia: maskini, wazee na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Bwana na bibi wanapoungana katika upendo wa dhati, baraka na matunda ya muungano huu ni watoto wanaopaswa kuwalinda, kuwahudumia na kuwaelimisha tunu msingi za imani na utu wema.

Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa watoto kuzaliwa na kupata malezi ndani ya familia inayoundwa na baba na mama na wala si kinyume chake. Huu ndio msimamo wa Mama Kanisa unaolenga kuwaimarisha waamini kusimama kidete dhidi ya utamaduni wa kifo na ubinafsi unaotaka kuhalalisha kila jambo kwa kisingizio cha uhuru na haki msingi za binadamu.

Askofu mkuu Cordileone anasema, kila mtu au kundi la watu linapaswa kuheshimiwa katika maamuzi yake, lakini maamuzi haya hayawezi kuvuruga msimamo na Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia. Kanisa litaendelea kusimamia kweli za Kiinjili na utu wema, kwa kuwataka waamini kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mguso bila ya kumezwa na malimwengu. Waamini wasimamie na kuutetea ukweli katika maisha yao ya kila siku.

Askofu mkuu Cordileone anasikitika kusema  kwamba, kuna baadhi ya watu wanalikashifu  Kanisa kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Familia, kwa vile tu, Kanisa halitaki kutambua ndoa za watu wa jinsia moja, jambo ambalo ni kinyume cha Mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu maisha ya ndoa na familia. Jamii inapaswa kujifunza kukubali na kuupokea ukweli; kukumbatia na kuheshimu kanuni maadili na utu wema badala ya kumezwa na malimwengu kwa kejeli za baadhi ya watu wanaotaka kukumbatia utamaduni wa kifo. Kabla ya kuhukumu, watu wajifunze kufahamiana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.