2015-03-26 10:56:00

Jubilee ya miaka 500 ya Mt. Theresa wa Avila, Siku ya kuombea amani!


Mama Kanisa tarehe 28 Machi 2015 anaadhimisha Jubilee ya miaka 500 tangu alipozaliwa Mtakatifu Theresa wa Avila, Bikira na Mwalimu wa Kanisa tukio ambalo linatarajiwa kuwaunganisha waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya sala kwa Mtakatifu Theresa wa Avila. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 26 Machi 2015 amezindua rasmi maadhimisho haya, kwa kuwaalika Wakarmeli, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kutenga muda wa saa moja kwa ajili ya kusali ili kuombea amani duniani.

Baba Mtakatifu anapenda kuungana na Wakarmeli wote kusali ili moto wa upendo wa Mungu ushinde nguvu ya moto wa chuki, vita na dhuluma unaoendelea kumwandama mwanadamu. Waamini wasali kweli majadiliano yapewe kipaumbele cha kwanza badala ya mtutu wa bunduki.

Padre Saverio CannistrĂ , Mkuu wa Shirika la Wakarmeli katika barua yake kwa wanashirika na watu wote wenye mapenzi mema anasema Mtakatifu Theresa wa Avila alikuwa daima anapiga kelele daima alipokuwa anaona vita inarindima sehemu mbali mbali za dunia; pale ambapo watu walitengana na kusambaratika kutokana na sababu mbali mbali kwa watu wa nyakati zake. Kwa njia ya imani na matumaini: vita, chuki na kinzani zinaweza kutoweka katika uso wa dunia, ikiwa kila mtu atajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kila siku.

Baba Mtakatifu anawaalika watu kutambua na kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia: Bado kuna: vita, kinzani, mashambulizi ya kigaidi, dhuluma na nyanyaso; ni wakati wa kusikiliza na kusimamisha kilio cha watu wasiokuwa na hatia. Huu ni wajibu msingi wa kila mtu. Tarehe 28 Machi ni siku ambayo Sala ya Mtakatifu Theresa wa Avila inapaswa kusikika katika mioyo ya watu, kwa kuombea amani duniani.

Ni kipindi cha waamini kukimbilia toba, wongofu na upatanisho. Ili amani ya kweli iweze kudumu katika mioyo ya watu kuna haja ya kujikita katika majadiliano, ukweli na uwazi sanjari na msamaha, ili kukimbilia huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.