2015-03-26 09:14:00

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Torino


Mateso na mahangaiko ya binadamu; ulimwengu wa vijana wa kizazi kipya na Jubilee ya miaka 200 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Bosco ni kati ya mambo makuu yatakayojiri wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, Jimbo kuu la Torino, Italia kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Juni 2015.

Haya yamefafanuliwa na Askofu mkuu Cesare Nosiglia, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Torino, wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Jumatano tarehe 25 machi 2015.  Hija ya Baba Mtakatifu Francisko inaongozwa na kauli mbiu “Upendo ni mkuu zaidi”. Padre Ciro Benedettini, msemaji mkuu msaidizi wa Vatican aliyeratibu mazungumzo haya anasema kwamba, hii itakuwa ni fursa makini kwa waamini kuanza kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu uliotangazwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu atakapowasili Jimboni Torino, atapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na ulimwengu wa wafanyakazi na wakulima. Atapata nafasi ya kusikiliza maswali kutoka kwa wafanyakazi, wakulima na wafabiashara. Baada ya hapo, Baba Mtakatifu atalekea kwenye Kanisa kuu na kusali mbele ya Altare ya Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati na baadaye, atasali pia kwa kitambo, mbele ya Sanda Takatifu, kielelezo cha mateso na mahangaiko ya mwanadamu.

Hapa Baba Mtakatifu anapenda kuungana na maelfu ya mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaotembelea Torino kila mwaka, ili kushuhudia Sanda Takatifu inayoonesha mateso ya Yesu Kristo. Sadaka na matoleo yote yatakayokusanywa wakati huu, yatatolewa kwa Baba Mtakatifu, kwa ajili ya kuchangia mshikamano wa kidugu na mapendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ibada ya Misa Takatifu ni kilele cha maadhimisho ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, Jimbo kuu la Torino. Baada ya maadhimisho haya, Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na maskini, wafungwa, watu wasiokuwa na makazi na wale wanaosukimizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kuonesha mshikamano wa dhati unaojikita katika utu na heshima ya binadamu na wala si kile alicho nacho mtu!.

Jioni, Baba Mtakatifu atatembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Consolata na kuzungumza na Mapadre wanaohudumia katika Madhabahu haya. Jimbo la Torino linataka kumuenzi pia Mtakatifu Yohane Bosco, wakati huu Kanisa linapoadhimisha Jubilee ya miaka 200 tangu alipozaliwa. Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuzungumza na Watoto wa Yohane Bosco pamoja na vijana wanaohudumiwa katika Parokia, kama sehemu muhimu sana ya majiundo ya vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu atawatembelea na kuwafariji wazee na wagonjwa.

Baba Mtakatifu akiwa Jimboni Torino atakutana pia na kuzungumza na vijana, ambao wanajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland, Julai 2016. Msalaba wa vijana kutoka Cracovia utakuwepo.

Baba Mtakatifu tarehe 22 Juni 2015 atatembelea Hekalu la Jumuiya ya Kikristo na kuzungumza pamoja na Wakristo  na baadaye atapata nafasi ya kusali na kula chakula cha mchana na ndugu pamoja na jamaa zake wa karibu. Jioni Baba Mtakatifu atasindikizwa na umati wa vijana kuelekea uwanja wa ndege wa Torino. Haya ndiyo yanayotarajiwa kujiri wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Jimbo kuu la Torino, kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Juni 2015.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kama kawaida, itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.