2015-03-25 08:19:00

Machozi ya Bikira Maria kwa ajili ya watoto wake!


Kuna idadi kubwa ya Wakristo wanaouwawa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na chuki za kidini kama hali inavyojionesha huko Syria, Iraq, Pakistan na Nigeria. Wote hawa wanaendelea kusindikizwa na kilio cha Bikira Maria kwa ajili ya watoto wake. Hayo yamesemwa na Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki wakati wa Ibada ya Masifu ya jioni kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Kitaifa ya Mariapocs, Jumanne tarehe 24 Machi 2015, wakati huu, Familia ya Mungu nchini Hungaria inapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka mia tatu tangu kujengwa kwa Madhabahu haya.

Bikira Maria anaendelea kulia na kuteseka moyoni mwake pale ambapo damu ya watu wasiokuwa na hatia inamwagika; pale watoto ambao bado hawajazaliwa wanatolewa mimba; analia pale ambapo anaona tunu bora za maisha ya ndoa na familia zinamong’onyoka na waamini wanaendelea kukengeuka. Bikira Maria anaendelea kutoa machozi ya uchungu anapoona watu wanamezwa na kugubikwa na utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao; pale wahamiaji wanapokufa maji kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania; anapoona mateso, nyanyaso na madhulumu ya Wakristo huko Mashariki ya kati.

Yote haya ni machozi ya Mama kwa watoto wake na kwamba, Bikira Maria anaendelea kumsindikiza binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani, kwa njia ya sala, ili aweze kuonja upendo na huruma ya Mungu. Kardinali Sandri anamwomba Bikira Maria kuwasaidia waamini kuchuchumilia huruma ya Mungu wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Kanisa halina budi kusonga mbele na mchakato wa Uinjilishaji, kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya Kikristo yanayomwilishwa katika furaha, amani na matumaini. Waamini nchini Hungaria wanaalikwa kwa namna ya pekee kusali kwa ajili ya kupata miito mitafakatifu ndani ya Kanisa; utakaowawezesha waamini hao kujisaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Leonardo Sandri na ujumbe wake wako nchini Hungaria kushiriki maadhimisho ya Jubilee ya miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Madhabahu ya Bikira Maria nchini humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.