2015-03-25 10:39:00

AMECEA na Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko, linaendelea kutafakari jinsi ya kukoleza umoja, udugu na ushirikiano kati ya mapadre na watawa katika mchakato wa ujenzi wa Familia ya Mungu inayowajibika Afrika Mashariki na Kati.

AMECEA katika mkutano wake wa mwanzo wa Mwaka 2015 uliofanyika hivi karibuni, Jijini Nairobi, umepembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo AMECEA inavyoweza kuadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, tukio la neema na baraka kwa pamoja, kama kielelezo cha shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa Mapendo kamili, “Perfectae caritatis”, changamoto ya kuyapyaisha maisha na utume wa watawa duniani. Itakumbukwa kwamba, Mwaka wa Watawa Duniani utafungwa rasmi hapo tarehe 2 Februari, 2016 wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani.

Mababa wa AMECEA wanasema kwamba, Mwaka wa Watawa Duniani ni kipindi cha neema na baraka tele si tu kwa watawa, bali kwa familia ya Mungu katika ujumla wake anasema Askofu John Oballa Owaa wa Jimbo Katoliki Ngong, Kenya. Watawa wanaojisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na watu, wanapaswa kuwa kweli ni kielelezo cha furaha, wema na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya huduma makini katika maisha na utume wao wa kitawa. Watawa waendelee kuwa ni mashuhuda wa kinabii katika ulimwengu mamboleo.

Askofu Oballa anasema, maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, iwe ni fursa ya kukoleza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na watawa kutoka katika Makanisa mengine ya Kikristo yaliyoko Afrika Mashariki na Kati. Ni fursa na mwaliko wa kukuza majadiliano kati ya watawa wa kizazi kipya na watawa wazee ambao wameonja upendo, ukarimu na tunza ya Mashirika yao, ili waweze kuwashirikisha watawa wa kizazi kipya mang’amuzi ya maisha, tayari kupambana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Watawa wanapaswa kuendelea kuwa waaminifu kwa karama za mashirika yao pamoja na Mashauri ya Kiinjili. Watawa wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika maisha na utume wao bila kugubikwa na ubaguzi wa tamaduni, rangi, kabila au mahali wanapotoka watawa hawa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa AMECEA.








All the contents on this site are copyrighted ©.