2015-03-24 09:27:00

Wananchi wa Kenya wanataka; ukweli na uwazi; haki na demokrasia


Ukweli na uwazi; demokrasia na utawala bora; ugavi na matumizi sahihi ya rasilimali ya Kenya ni kati ya mambo ambayo yanapewa kipaumbele cha kwanza na Tume ya haki na amani Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya, ili kujenga misingi ya utawala bora, unaojali na kuzingatia ustawi na mafao ya wengi. Wananchi wa Kenya wanapaswa kufahamu jinsi ambavyo rasilimali ya taifa inavyotumika na kuchangia katika maendeleo endelevu ya Wakenya bila kujali tofauti zao msingi.

Ukosefu wa uwiano sawa wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchochea kinzani za kijamii kati ya wakulima na wafugaji na wakati mwingine, kinzani hizi zinajikita katika ukabila na udini kwa baadhi ya maeneo. Hali hii imepelekea kwa kiasi kikubwa ukosefu wa fursa za ajira na umaskini kwa baadhi ya maeneo nchini Kenya kutokana na ukweli kwamba, sera na mikakati mingi ya maendeleo haikutekelezwa kama ilivyopangwa.

Tume ya haki na amani, inaiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba, inatoa habari muhimu kwa wananchi wake, kama sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya utawala bora; wananchi wafahamu na kuchangia katika ustawi wa nchi yao kwa njia ya demokrasia inayojikita katika uwakilishi katika sehemu mbali mbali za maamuzi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Kuna haja ya kuwa makini na matumizi ya fedha ya umma, ili ilete maendeleo yanayokusudiwa badala ya mtindo wa sasa wa kuwanufaisha baadhi ya wafanyakazi Serikalini. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa Katoliki nchini Kenya linapenda kuchangia kwa hali na mali katika mchakato wa kuwaletea wananchi wa Kenya maendeleo endelevu; kwa kukazia demokrasia inayosimikwa katika ukweli na uwazi, ustawi na mafao ya wengi; utu na heshima ya binadamu. Taasisi za demokrasia na maendeleo ya watu hazina budi kuimarishwa pamoja na kuhakikisha kwamba, wananchi wote wanashiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo.

Ili kufanikisha yote haya kuna haja kwa wananchi wa Kenya kujenga utamaduni wa majadiliano, ili kweli Kenya iweze kucharuka: kiuchumi, kijamii na kisiasa, ndoto ambayo inawashirikisha wananchi wengi wa Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.