2015-03-24 12:02:00

Wamissionari waliouwawa kikatili tangu mwaka 1980-2014 ni 1, 062


Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema kwamba, idadi ya Wakristo wanaoendelea kumwaga damu yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa miaka ya hivi karibuni imeongezeka maradufu. Mama Kanisa nchini Italia, tarehe 24 Machi ya kila mwaka anaadhimisa Siku ya Wamissionari Mashahidi, walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Upendo, Matumaini na Mshikamano wa dhati. Katika kipindi cha miaka thelathini na mitano iliyopita, Wamissionari 1, 062 wameuwawa kutokana na chuki za kiimani na ukatili, sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa linamkumbuka pia mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Oscar Romero aliyeuwawa kikatiliki miaka thelathini na tano iliyopita.

Hii ni siku ya kufunga na kusali kwa ajili ya Wamissionari wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kutangaza  Habari Njema ya Wokovu. Takwimu zinaonesha kwamba, kati ya mwaka 1980 hadi mwaka 1989, Wamissionari 115, waliuwawa kikatili sehemu mbali mbali za dunia. Kati ya Mwaka 1990 hadi mwaka 2000 idadi ya Wamissionari waliouwawa ilikuwa ni 604, idadi hii ni kubwa zaidi kutokana pia na mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda na kupelekea Wamissionari 248 nchini humo kuuwawa kikatiliki.

Kati ya Mwaka 2001 hadi mwaka 2014 Wamissionari waliouwawa ni 343. Na katika kipindi cha mwaka 2014 watumishi wa Kanisa 26 waliuwawa. Shirika la Habari za Kimissionari Fides linabainisha kwamba, idadi hii pengine ni kubwa zaidi, kwani takwimu zilizotolewa ni kwa baadhi ya maeneo na katika mazingira maalum.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.