2015-03-24 09:52:00

Miaka 35 tangu alipouwawa kikatili Askofu mkuu Oscar Romero


Mama Kanisa anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 35 tangu Mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Oscar Arnufo Romero alipouwawa kikatili kunako tarehe 24 Machi 1980 wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la San Salvador, nchini El Salvador. Anatarajiwa kutangazwa kuwa Mwenyeheri hapo tarehe 23 Machi 2015 huko San Salvador.

Kardinali Vincent Nichols, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Westminster katika Ibada ya Misa takatifu amemkumbuka Mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Oscar Romero aliyetoa kipaumbele cha pekee katika kwa maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana hali yao ya maisha. Alikuwa msikivu kwa kilio, mateso na mahangaiko yao, na kuwatimizia kadiri ya uwezo wake, kiasi cha kujikita katika mioyo ya maskini na maskini wakamkubali na kumkumbatia kama Baba na mchungaji wao mwema.

Askofu mkuu Romero akauwawa kutokana na chuki za kiimani, chuki dhidi ya Yesu Kristo na Kanisa lake. Ni kiongozi aliyeonesha kwamba, upendo wa Mungu ni chemchemi ya utu na heshima ya binadamu. Kwa watu wanaobeza utu na heshima ya binadamu wanaishia kukengeuka na ukanimungu. Askofu mkuu Romero ni kielelezo cha umoja na mshikamano katika Kristo, changamoto ya kuendeleza umoja miongoni mwa Wakristo sanjari na kushikamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani hii ni hazina na amana ya Kanisa.

Ufukara uwawezeshe watu kuonja shida na mahangaiko ya jirani zao, kwa kukubali kupokea Msalaba, ili kuendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.