2015-03-24 12:37:00

Iweni Wakristo imara, thabiti na jasiri


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne, tarehe 24 Machi 2015 anawataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kwa kuonesha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa linahitaji watu wenye msimamo thabiti, wasiyoyumbishwa na pepo za mpito!

Ni changamoto ya kuendelea kujivika neema na baraka zinazowamiminikia kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ili kukumbatia neema na wokovu pasi na kunung’unika kama walivyokuwa Waisraeli kwenye Agano la Kale, waliosababisha hata Mwenyezi Mungu akawaonjesha chamtema kuni kwa kumtuma nyoka awang’ate! Lakini bado anawaonea huruma kutokana na sala na maombezi ya Nabii Musa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema Waisraeli walikinai kula manna iliyokuwa inashuka kutoka mbinguni, wakafundishwa adabu na kuoneshwa nyoka wa shaba, alama ya Msalaba wa Kristo anayemwokoa mwanadamu kutokana na sumu ya nyoka! Hata leo hii kuna Wakristo wanaoendelea kulalamika na kumnung’unikia Mwenyezi Mungu katika maisha yao; wanashindwa kuinua macho yao mbinguni ili kukimbilia wokovu unaoletwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Msalaba.

Ni watu wasiokuwa na uhakika wa hija ya ukombozi katika maisha yao. Sumu ya kumkinai Mungu ni dhambi inayomwondolea mwamini furaha na hatimaye kushindwa kuandamana na Yesu katika Njia ya Msalaba.  Yesu aliyeinuliwa juu Msalabani, amechukua dhambi za binadamu, mwaliko kwa waamini kufia dhambi kutoka katika giza la maisha yao ya kiroho, kwa kuondokana na manung’uniko la malalamiko yasiyokuwa na tija hata kidogo katika ustawi na maisha ya kiroho.

Yesu ndiye Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu na wana heri wale wanaomkubali na kukimbilia wokovu wake. Waamini wawe na ujasiri wa kupokea njia na mwongozo unaoletwa kwao na Yesu Kristo, ili waweze kuwa ni Wakristo shupavu na jasiri katika maisha na utume wao anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.