2015-03-23 08:59:00

Waonesheni: Injili, Msalaba na ushuhuda wa maisha


Mwinjili Yohane, Jumapili ya tano ya Kwaresima, kama sehemu ya maandalizi ya Siku kuu ya Pasaka, anawaonesha kwa namna ya pekee, Wayunani waliotaka kumwona Yesu. Ikumbukwe kwamba, kuna watu wa kawaida kabisa waliomkubali na kumpokea Yesu wa Nazareti kuwa Nabii aliyetumwa na Mungu. Lakini kuna Mafarisayo na Makuhani wakuu wanataka kumng’oa Yesu miongoni mwao kwani walimwona kuwa ni mtu hatari na aliyekuwa anawapotosha watu.

Kulikuwepo pia na watu waliokuwa na udadisi wa kutaka kumwona, kumfahamu na kuzungumza na Yesu kama ilivyotokea kwa Wayunani wanaotajwa na Mwinjili ya Yohane. Walitaka kusikia na kuona matendo makuu yaliyotendwa na Yesu, kati ya matendo haya ni ufufuko wa Lazaro, tukio ambalo liliwaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi.

Hamu ya kutaka kumwona Yesu, anasema Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Jumapili tarehe 22 Machi 2015 ni hamu ambayo imeoneshwa na watu wa nyakati na tamaduni mbali mbali. Ni hamu ambayo inapata chimbuko lake kutoka katika undani wa watu waliosikia habari kuhusu Yesu, lakini walikuwa hawajabahatika kukutana naye uso kwa uso.

Yesu anawajibu kwa mtindo wa Kinabii, kwa kufunua utambulisho wake na kuonesha ile Njia ya Msalaba ambayo Mwana wa mtu anaifuata, ili aweze kutukuzwa. Hii ndiyo Saa ya Msalaba, muda wa kumshinda Shetani na kudhihirisha upendo na huruma ya Mungu. Yesu anasema, akishainuliwa juu, yaani akisha tundikiwa juu Msalabani, atafufuka na kupaa kwenda mbinguni; huko atawavuta wengi kwake, ili waweze kujipatanisha na Mungu na kati yao! Saa ya Msalaba ni tukio la giza katika historia, lakini ni chemchemi ya wokovu kwa wale wanaomwamini Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, Yesu anaonesha kwamba, kifo chake ni sawa na mbegu ya ngano ambayo ikizikwa ardhini itazaa matunda mengi, kwani kifo cha Yesu ni chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka katika upendo wa Mungu. Wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanaweza kuwa ni mbegu ya ngano kwa kujasadaka maisha yao kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani.

Kwa wale wote wanaotaka kumwona Yesu na wale wanaotafuta uso wa Mungu, wale ambao pengine walipokea imani wakiwa na umri mdogo na kwa sasa wamepoteza imani hiyo pamoja na umati mkubwa wa watu ambao bado haujabahatika kumwona Yesu; Wakristo wanaweza kuwazawadia mambo makuu matatu: Injili, Msalaba na Ushuhuda. Kwa njia ya Injili, waamini wanaweza kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao, kwa kumsikiliza na hatimaye, kumfahamu. Msalaba ni kielelezo cha upendo mkuu wa Yesu aliyejisadaka kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ushuhuda wa Kikristo unapaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma na kidugu; sanjari na uhalisia wa maisha; kwa maneno, lakini kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.