2015-03-23 09:59:00

Siku ya Maji Duniani 2015


Maji na maendeleo endelevu ndiyo kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani kwa Mwaka 2015, iliyofanyika, Jumapili tarehe 22 Machi 2015. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika tafakari kuhusu umuhimu wa maji katika maisha ya mwanadamu linabainisha kwamba, maji ni sehemu muhimu sana katika maisha, ustawi na maendeleo endelevu ya mwanadamu.

Maji ni chemchemi ya uhai kwa viumbe vyote duniani na kwamba, hii ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu ambayo haina mbadala. Hii ni changamoto ya kulinda, kutunza na kuendeleza vyanzo vya maji kwani ni chemchemi ya uhai na vinasaba vya binadamu. Mwanadamu anazaliwa na maji na kwamba, maji hayana mbadala na kamwe hayawezi kugeuzwa kuwa ni sawa na bidhaa nyingine zote.

Hii ndiyo maana, Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema kwamba, maji hayapaswi kubinafishwa kwani hii ni mali ya umma inayopaswa kutumiwa kwa uwajibikaji mkubwa na kwa ajili ya mafao ya wengi. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendesha kampeni ya haki ya maji duniani, kwa njia ya tafakari, sala na makongamano mbali mbali ili kuwasaidia watu kufahamu umuhimu wa haki ya maji, tayari kuiendeleza kikamilifu.

Mji ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu yanayozingatia mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Bila maji, maisha ya mwanadamu yako hatarini. Maji ni chanzo cha nishati, uzalishaji na huduma katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu na kigezo muhimu sana cha ustawi na maendeleo ya kweli.

Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani, iwe ni fursa endelevu inayopania kusaidia mchakato wa maboresho ya huduma ya maji safi na salama, kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia. Umoja wa Mataifa unatarajia hapo mwezi Septemba 2015 kuzindua kampeni inayopania kutoa kipaumbele cha pekee katika upatikanaji wa maji safi na salama.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.