2015-03-23 09:11:00

Maji ni uhai


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 22 Machi 2015 aliipongeza na kuishukuru Familia ya Mungu Jimbo kuu la Napoli, ambako mwishoni mwa juma alipata nafasi ya kuwatembelea, kusali na kuzungumza nao kwa muda wa masaa kumi. Amewashukuru kwa moyo wa ukarimu na mapendo waliomwonesha wakati wa hija yake ya kichungaji Jimboni humo.

Baba Mtakatifu amewapongeza watu wote walioshiriki katika mbio za Marathoni zilizofanyika mjini Roma kwa ujasiri na ushujaa waliouonesha katika kuchanja mbuga, kwani licha ya hali mbaya ya hewa, lakini watu wengi wamejitokeza na kushiriki kikamilifu.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko amekumbusha kwamba, tarehe 22 Machi 2015, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Maji Duniani. Maji ni uhai na kwamba, utunzaji bora wa maji ni changamoto kubwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu kwa siku za usoni.

Baba Mtakatifu anaitia shime Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inalinda na kutunza vyanzo vya maji sehemu mbali mbali za dunia, ili maji haya yaweze kutumiwa vyema na hasiwepo mtu anayetengwa wala kubaguliwa kutumia maji, ambayo ni kwa ajili ya mafao ya wengi. Mtakatifu Francisko katika utenzi wake wake anatoa sifa kuu ya maji kwa kutambua umuhimu wake katika maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, amewagawia waamini waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican zawadi ya Injili kama ilivyo desturi kwa Mama Kanisa, Jumapili ya tano ya Kwaresima kuwapatia Wakatekumeni Injili, kama sehemu ya maandalizi ya kuadhimisha Fumbo la Pasaka.

Zawadi hii ya Baba Mtakatifu imesambazwa na watu wasiokuwa na makazi maalum mjini Roma. Mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kujisomea, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu kama kielelezo cha imani tendaji. Waamini wanakumbushwa kwamba, Neno la Mungu ni taa inayowaangazia mapito yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.