2015-03-23 09:49:00

Changamoto za mawasiliano Barani Afrika


Mkutano mkuu wa Umoja wa Watangazaji Barani Afrika, AUB, uliokuwa unafanyika mjini Dakar, Senegal, umekamilika kwa kutoa tamko ambalo linaonesha umuhimu wa chombo hiki kuendelea kujikita katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko kutoka katika matumizi ya teknolojia ya analogia kuelekea teknolojia ya digitali, kama sehemu ya upyaisho wa huduma inayotolewa na vituo vya Radio na Televisheni Barani Afrika.

Hii ni changamoto inayojikita katika masuala ya kiuchumi, kifedha na kijamii, mwaliko kwa nchi wanachama kushikamana na kushirikiana kwa karibu zaidi katika kubadilishana teknolojia na vipindi mbali mbali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.

Wajumbe wameridhika na changamoto iliyotolewa na viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika katika kusaidia mchakato wa mabadiliko ya teknolojia, ili kwenda na wakati pamoja na kuhakikisha kwamba, vituo vya Radio na Televisheni Barani Afrika vinatoa huduma bora zaidi kwa ajili ya wananchi wa Bara la Afrika. Wizara zinazohusika na masuala ya habari na mawasiliano ya jamii Barani Afrika hazina budi kuhakikisha kwamba, zinaratibu mabadiliko haya, ili kusaidia shughuli za ufanisi wa mawasiliano Barani Afrika pamoja na kuendelea kushirikiana na AUB kwa karibu zaidi.

Wajumbe walibainisha kwamba, kuna haja kwa AUB na ATU kushirikiana  kuunda kamati itakayounda jamii ya mawasiliano inayowahusisha pia watengenezaji na wafanyabiashara wa vifaa vya mawasiliano ya jamii, ili kusaidia harakati za kufufua uchumi Barani Afrika.

Wajumbe pia wamegusia umuhimu wa kudhibiti masafa ya matangazo kwa kushirikiana na wadau wengine katika nchi husika. Wajumbe pia walifanya uchaguzi kwa kamati mbali mbali ili kurahisisha masuala ya uongozi na utekelezaji wa majukumu yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.