2015-03-23 10:08:00

Bikira Maria, Utuombee


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kuanzia tarehe 22 hadi 25 Machi 2015 yuko nchini Hungaria kwa mwaliko wa Maaskofu Wagriki Wakatoliki wakati huu wanapoadhimisha Jubilee ya miaka mia tatu tangu kuanzishwa kwa Madhabahu ya Bikira Maria kitaifa pamoja na kutabaruku Kanisa kuu la Miskolc.

Akiwa nchini humo, Kardinali Sandri na ujumbe wake wanashiriki katika maadhimisho ya Madhabahu ya Bikira Maria, maarufu sana kwa waamini kutoka ndani na nje ya Hungaria. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 18 Agosti 1991 alitembelea Madhabahuni hapo na kusali pamoja na waamini.

Ratiba inaonesha kwamba, tarehe 25 Machi 2015, Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, Kardinali Sandri anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria sanjari na kutabaruku Kanisa kuu la Miskolc.

Hii itakuwa ni nafasi kwa Kardinali Sandri kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Hija hii ya kitume inafanyika baada ya marekebisho makubwa yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuunda Jimbo kuu, ili kusogeza huduma za kichungaji kwa Familia ya Mungu nchini humo. Ni muda wa kusali kwa ajili ya kuliombea Kanisa pamoja na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.